1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Trump wazoa ushindi kinyang´anyiro cha ´Jumanne Kuu´

6 Machi 2024

Matokeo ya kura ya mchujo iliyofanyika siku ya Jumanne kwenye zaidi ya majimbo 15 ya Marekani yanaendelea kutolewa huku Rais Joe Biden na mpinzani wake Rais wa zamani Donald Trump wakijizolea ushindi wa majimbo mengi.

https://p.dw.com/p/4dCtN
Marekani | Kura za mchujo
Kura za mchujo nchini Marekani Picha: Allison Joyce/AFP/Getty Images

Kura hiyo ya mchujo ndiyo itakayoamua wanasiasa watakaopeperusha bendera ya vyama vikuu viwili katika uchaguzi wa rais nchini Marekani utakaofanyika mwezi Novemba.

Rais Joe Biden kutoka chama cha Democratic anawania muhula wa pili bila ushindani wowote mkubwa na inatazamiwa ndiye atakuwa mgombea wa chama hicho.

Kwa upande wa Republican, rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ndiye anapigiwa upatu wa kuwa tena mgombea, katika kile kinatazamwa kuwa uwekano wa mpambano mwingine kati yake na Biden aliyemshinda mwaka 2020.

Hadi mapema asubuhi, Biden tayari alikuwa ametangazwa mshindi kwenye majimbo kadhaa yaliyoshiriki kura ya mchujo ya jana Jumanne inayofahamika kama "Kinyang´anyiro cha Jumanne Kuu".

Biden ameshinda majimbo ya Oklahoma, Virginia, Tennesee, North Carolina, Vermont na Iowa. Mengine ni Maine, Utah, Minnesota, Texas na Massachusetts.

Trump azoa majimbo mengi zaidi akimpiga kumbo mpinzani wake mkuu, Nikki Haley 

Trump alishinda jimbo la South Carolina, nyumbani kwa mpinzani wake Nikki Haley.
Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, amekuwa akipata ushindi katika karibu kila jimbo lililokwishafanya kura ya mchujo ikiwemo jimbo la South Carolina, nyumbani kwa mpinzani wake Nikki Haley.Picha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake Trump naye amepata ushindi kwenye majimbo ya Oklahoma, Virginia, Tennesee, North Carolina na Maine akimbwaga kwa mara nyingine kwa wingi mkubwa wa kura mpinzani pekee aliyebakia, Nikki Haley. Ametangazwa pia mshindi huko Massachusetts,Texas, Colorado na Alabama.

Tangu kuanza kwa kura za mchujo kwenye majimbo ya Marekani mnamo katikati ya mwezi Januari, Trump ameshinda majimbo yote ikiwemo South Carolina ambalo ni jimbo la nyumbani kwa Nikki Haley.

Mapema wiki hii Haley alipata ushindi wa kwanza na unaozingatiwa kuwa mdogo kwa kuinyakua wilaya ya Washington D.C.

Matokeo ya kura za mchujo yanayoendelea kutolewa huenda yataongeza shinikizo kwa Haley -- balozi wa zamani wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa-- kutangaza kujiondoa katika kinyang´anyiro cha kuwania urais.

Iwapo hilo litatokea, macho na masikio yataelekezwa kwa Biden na Trump, wanasiasa wawili wenye umri mkubwa ambao wameshindwa kuibua msisimko miongoni mwa wapigakura wa Marekani kuelekea uchaguzi wa rais.

Uhamiaji, hali ya uchumi na mzozo wa Gaza masuala muhimu uchaguzi wa Novemba 

Trump| Biden
Rais Joe Biden na Donald Trump huenda watachuana tena kwenye uchaguzi wa rais mnamo Novemba, 2024.Picha: ABACA/IMAGO;AP Photo/picture alliance

Uchunguzi wa maoni ya umma unaonesha Wamarekani wangependelea chaguo jingine katika uchaguzi wa mwaka huu badala ya Trump na Biden. Hata hivyo ishara zote zinaonesha watawalazimika kuchagua miongoni mwa wagombea hao wawili.

Pamoja na ushindi wa kura za jumanne kuu, Trump atasubiri hadi Machi 12 kufahamu iwapo ametimiza idadi ya wajumbe wanaohitajika ili kujihakikishia kwamba atakuwa mgombea wa chama cha Republican. Kwa upande wa rais Biden, tarehe hiyo inayosubiriwa ni Machi 19.

Masuala makubwa katika uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka huu, itakuwa ni uhamiaji, hali ya uchumi na taathira ya vita vya Gaza.

Trump anautuhumu utawala wa Biden kwa kushindwa kuzuia wimbi kubwa la wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati akisema sera yake ya kudhibiti wahamiaji ndiyo inahitajika sasa nchini Marekani.

Biden anajisifu kuwa hali ya uchumi imeimarika ikiwa ni pamoja na kuongeza nafasi za kazi na kuepusha mdodoro baada ya kurithi janga la virusi vya corona alipoingia madarakani mwaka 2021.