BAYERN MUNICH YAPIGWA KUMBO NJE YA CHAMPIONS LEAGUE | Michezo | DW | 12.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

BAYERN MUNICH YAPIGWA KUMBO NJE YA CHAMPIONS LEAGUE

AC Milan imeinyoa jana B.Munich kwa mabao 2 bila ya maji.Sasa imeweka midai ya nusu-finali na Manchester United ilioitimua nje AS Roma ya Itali kwa mabao 7-1.Liverpool imeilaza PSV Eindhoven kwa bao 1:0.

Baada ya changamoto za jana za champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya,nusu-finali ya kombe hilo itakua kati ya timu za Uingereza-Manchester United,Chelseana Liverpool dhidi ya timu moja ya Itali-AC Milan waliowachezesha jana mabingwa wa Ujerumani- Bayern Munich kindumbwe-ndumbwe na kuitoa kwa mabao 2:0.

Leo ni zamu ya Bayer Leverkusen –klabu ya mwisho ya Ujerumani katika kombe la Ulaya msimu huu ikicheza na Ousasuna ya Spian.Na baada ya kukandikwa mabao 3:0 nyumbani duru ya kwanza, Leverkusen leo nayo yaweza kuaga kombe la UEFA:

FC Liverpool jana ilizifuata timu 2 za Uingereza-Manchester United iliokongoa meno AS Roma kwa mabao 7-1 hapo juzi kwa kuitimua PSV Eindhoven ya Holland kwabao la Peter crouch na kutoroka na tiketi ya tatu ya timu za Premier League katika nusu-finali ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya.Jana usiku AC Milan ya Itali ikaupiga msumari wa mwisho katika jeneza la mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich ilipowazaba mabao 2:0.

Bao la Clarance Seedorf na Inzaghi yaliopachikwa mnamo muda wa dakika 5 za kipindi cha kwanza yalitosha kuichimbia kaburi na kuizika Munich uwanjani mwao Allianz Arena.

Sasa kocha wa AC Milan Carlo Ancelotti amezionya timu 3 za Uingereza kuwa AC Milan imepania kufuta aibu waliopakwa wataliana juzi pale Manchester ilipoirarua AS Roma kwa mabao 7:1.AC Milan ina miadi na Manchester United katika duru ya kwanza ya nusu-finali hapo April 24 na duru ya pili mjini Milan Mei 2.

Kocha wa Bayern Munich, Ottmar Hitzfeld ameungama kwamba timu yake imevunjika moyo sana kwa pigo la jana usiku.Kwani rekodi ya Bayern Munich ya kushinda nyumbani mara 11 katika champions League ilivunjwa jana na AC Milan-rekodi walioiweka tangu Novemba 2004.Duru ya kwanza Milan na Munich zilitoka suluhu 2:2 na Munich ikicheza jana nyumbani ilihisi jogoo la shamba-Milan lisingewika mjini Munich.Lakini,limewika.

Kocha Hitzfeld asema:

“Leo tumecheza na timu adui kali kabisa ambae alituzidi nguvu mno.Kwahivyo, hatukuvunjika moyo sana kana kwamba tulikuwa na tama ya kubadili mkondo wa mchezo sekunde ya mwisho.”

Nae kipa wa Bayern Munich,Oliver Kahn akiwatolea saluti na heko AC Milan kwa ushindi wa jana alisema:

“Nimejioneab leo timu bora kuliko zote barani ulaya.Nimecheza na timu nyingi kali tena kwa miaka mingi.AC Milan wanacheza kwa ufundi wa hali ya juu kabisa na nionavyo mimi , hii ndio timu itakayotawazwa mabingwa msimu huu.”

Finali ya champions League msimu huu itakua kati ya timu pekee za Uingereza au wataliana watawatilia waingereza kitumbua chao mchanga?

Tarakimu za zamani za Kombe hili zaonesha finali Mei 23 mjini Athens,itaaniwa na timu 2 zaote kutoka Uingereza.Lakini, hata AC Milan,historia ya kombe hili ipo upande wao watakapokutana na Manchester katika nusu-finali.

Kwahivyo, changamoto ni kati ya timu 3 za Uingereza-Manu,Chelsea,Liverpool dhidi ya 1 ya Itali, AC Milan.

 • Tarehe 12.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHcO
 • Tarehe 12.04.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHcO