1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Greenfield kukutana na wakimbizi wa Sudan huko Chad

Grace Kabogo
6 Septemba 2023

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, leo amewasili Chad ambako atakutana na wakimbizi wa Sudan waliokimbia machafuko ya kikabila na unyanyasaji wa kingono huko Darfur.

https://p.dw.com/p/4W0XH
Wakimbizi wa Sudan
Wakimbizi wa Sudan waliokimbilia ChadPicha: Marie-Helena Laurent/WFP/AP/picture alliance

Greenfield atalizuru eneo la Chad linalopakana na Darfur, magharibi mwa Sudan kwa lengo la kuangazia mgogoro unaozidi kuwa mbaya na kuongezeka kwa mzozo wa kibinadamu kutokana na kuzuka kwa mapigano mapya Aprili 15.

Umoja wa mataifa waomba msaada wa dola bilioni moja kuwasaidia wasudan

Akizungumza kabla ya kuwasili Chad, mjumbe huyo wa Marekani amesema wameshuhudia kiwango kikubwa cha ukatili unaofanywa, na mapigano hayo yanakumbushia kile walichokiona mwaka 2004, ambapo ilisababisha Marekani kutangaza kuwa mauaji ya kimbari.

Greenfield amesema wamesikia taarifa za wanawake wanaobakwa mara kwa mara, vijiji kuvamiwa na kuchomwa na makaburi ya watu wengi.

Balozi wa Marekani Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-GreenfieldPicha: John Lamparski/NurPhoto/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema tangu kuanza kwa vita vya Sudan mwezi Aprili, wkaimbizi wapatao 380,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekimbilia Chad. Maelfu wengine wamekimbilia Jamhuri ya Afrika ya Kati, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.

Shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeomba msaada wa dola bilioni moja kwa ajili ya kuwasaidia zaidi ya watu milioni 1.8 ambao wanatarajia kuikimbia Sudan ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, huku kukiwa na ripoti za ongezeko la kasi ya maambukizi ya magonjwa na vifo.

Naye mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu na masuala ya dharura, Martin Griffiths, amesema kwa mara nyingine tena Darfur imekuwa eneo ambalo halina huruma waka matumaini. Katika taarifa yake, Griffiths amesema watu wamekwama, wanalengwa, wanabakwa na wanauawa. Amesema matukio yote haya ni kinyume cha sheria na yanatisha.

Soma pia: Je kikosi cha Umoja wa Ulaya kitafaulu kuwalinda wakimbizi nchini Chad

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wahamiaji IOM, limesema takriban watu milioni 7.1 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini Sudankutokana na vita vya mwaka huu.

Kambi ya wakimbizi ya Zabout huko Chad
Wakimbizi wa Sudan katika kambi ya Zabout huko ChadPicha: Pierre Honnorat/WFP/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa IOM, zaidi ya asilimia 50 ni watu wapya waliolazimika kuyahama makaazi yao kutokana na vita hivyo. Shirika hilo limesema juhudi za kimataifa za kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Sudan zimeshindikana. Pamekuwepo na makubaliano yaliyofikiwa mara tisa ya kusitisha mapigano tangu vita vilipozuka, lakini yote yamevunjika.

Vita vya hivi karibuni vya Sudan Sudan vimezuka miaka minne baada ya rais wa zamani Omar al-Bashir kuondolewa madarakani, kati ya jeshi la Sudan SAF, na Kikosi Maalum cha Wanamgambo wa RSF.