1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bahrain yaungana na UAE kurejesha uhusiano na Israel

Tatu Karema
12 Septemba 2020

Bahrain siku ya Ijumaa 11.09.2020 ilijiunga na Muungano wa falme za kiarabu katika kukubali kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Israeli hatua iliyochochewa kiasi na hofu ya pamoja kuhusu Iran .

https://p.dw.com/p/3iMeZ
Bahrain l König Hamad bin Isa al-Chalifa in Manama
Picha: picture alliance/dpa/R. Jensen

Ikulu ya White House nchini Marekani imesema rais Donald Trump alitoa tangazo hilo kupitia ukurasa wake wa twitter baada ya kuzungumza kwa njia ya simu na mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Al Khalifa na waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu.Akiwahutubia wanahabari katika ofisi yake, Trump aliitaja siku hiyo kuwa ya kihistoria na kwamba anaamini mataifa mengine yatafuata mkondo huo.

Katika taarifa ya pamoja, Marekani, Bahrain na Israeli zimesema kuwa kufungua mawasiliano ya moja kwa moja na ushirikiano kati ya pande hizo mbili na chumi zilizoimarika kutaendelea kuleta mabadiliko ya manufaa katika eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza uthabiti, usalama na ufanisi katika eneo hilo.

Hofu ya Wapalestina

Wapalestina walifadhaika, wakihofia kuwa hatua hiyo ya  Bahrain na Muungano wa Falme za Kiarabu itadhoofisha msimamo wa muda mrefu wa mataifa ya kiarabu unaoitaka Israeli kuondoka katika makazi iliyokalia na kukubali utaifa wa Palestina kabla ya kurejelea uhusiano wa kawaida na mataifa ya Kiarabu.

Mwezi uliopita, Muungano wa Falme za Kiarabu ulikubali kurejesha uhusiano wa kawaida na Israeli chini ya mkataba uliosimamiwa na Marekani unaotarajiwa kutiwa saini katika sherehe itakayoandaliwa katika ikulu ya White House siku ya Jumanne, itakayoongozwa na rais Trump anayetafuta kuchaguliwa tena kama rais katika uchaguzi wa Novemba 3. Sherehe hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na waziri wa mambo ya nje wa Muungano wa Falme za Kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahyan.

Israel Benjamin Netanjahu Friedensvertrag mit Vereinigten Arabischen Emiraten
Benjamin Netanyahu- waziri mkuu wa IsraelPicha: Reuters/A. Sultan

 

Taarifa hiyo ya pamoja pia ilisema kuwa waziri wa mambo ya nje wa Bahrain Abdullatif Al Zayani pia atahudhuria sherehe hiyo na kutia saini ''azimio la kihistoria la amani'' na Netanyahu. Netanyahu amesema kuwa uamuzi wa Bahrain unaadhimisha ''enzi mpya ya amani.'' Katika taarifa iliyotolewa kwa njia ya video, Netanyahu alisema,'' Kwa miaka mingi tumewekeza katika amani na sasa amani itawekeza kwetu na kuleta uwekezaji mkubwa katika uchumi wa Israeli''.

Wito wa Palestina kwa Bahrain

Taarifa iliyotolewa chini ya jina la uongozi wa Palestina uliyatuhumu makubaliano hayo na kuyataja kuwa usaliti kwa azma ya Palestina. Taarifa hiyo ilisema, '' Uongozi wa Palestina unapinga hatua iliyochukuliwa na ufalme wa Bahrain na kuutaka kujiondoa katika makubaliano hayo mara moja kutokana na madhara makubwa itakayowaletea raia wa Palestina na hatua za pamoja za mataifa ya Kiarabu. Wizara ya mambo ya nje ya Palestina imesema kuwa balozi wa Palestina kwa Bahrain aliitwa tena kwa mashauriano.

Katika ukanda wa Gaza, msemaji wa kundi la Hamas Hazem Qassem alisema uamuzi wa Bahrain wa kurejelea uhusiano wa kawaida na Israeli ''unaashiria madhara makubwa kwa azma ya Palestina.'' Hossein Amir-Abdollahian, mshauri maalumu wa masuala ya kimataifa wa spika wa bunge la Iran, aliutaja uamuzi wa Bahrain kuwa usaliti mkubwa kwa azma ya mataifa hayo ya kiislamu na Palestina.

Marekani, Israeli na Muungano wa falme za Kiarau zimeihimiza Palestina kurejelea mazungumzo yake na Israeli. Mazungumzo  kati ya Israeli na Palestina yalikwama mara ya mwisho mnamo mwaka 2014 na rais wa Palestina Mahmoud Abbas amekataa uhusiano wowote wa kisiasa na serikali ya Trump kwa zaidi ya miaka miwili akiituhumu kwa kuipendelea Israeli.