BAGHDAD: Marekani na Iran zakutana kwa mara kwanza katika kipindi cha miaka 27 | Habari za Ulimwengu | DW | 28.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

BAGHDAD: Marekani na Iran zakutana kwa mara kwanza katika kipindi cha miaka 27

Mabalozi wa Marekani na Iran wanakutana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 27 mjini Baghdad kujadili machafuko yanayoendelea kuongezeka baina ya Wasunni na Washia.

Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Marekani na Iran ulikatika mnamo mwaka wa 1980 mwaka mmoja baada ya ubalozi wa Marekani mjini Tehran kushambuliwa kwenye mapinduzi ya kiislamu.

Mkutano wa mjini Baghdad unawaleta pamoja balozi wa Marekani nchini Irak, Ryan Crocker, na balozi wa Iran nchini humo, Hassan Kazemi.

Balozi wa zamani wa Marekani nchini Irak, Zalmay Khalilzad, amesema ipo haja ya kusubiri mabadiliko yatakayotokea nchini Irak.

´Itatubidi tusibiri mabadiliko yatakayotokea kuhusu silaha zinazoingizwa kupitia mpakani, misaada kwa makundi ya wapiganaji, watu wanaovuka mipaka kuja kuwasaidia waasi na makundi mengine yasiyo halali yaliyojihami na silaha. Haya ni maswala yanayotakiwa yachunguzwe kitabia, jambo ambalo ni muhimu katika kipindi kirefu.´

Waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki, amesema serikali yake ingependelea Marekani na Iran zisuluhishe tofauti zao katika mazungumzo hayo.

Makamanda wa Marekani nchini Irak wanaishutumu Iran kwa kuwaletea silaha wapiganaji nchini Irak na kuwadhamini wanamgambo wa kishia.

Iran kwa upande wake inapinga hatua ya Marekani kuikalia Irak na inaishutumu Marekani kwa kuendeleza mtandao wa ujasusi nchini Iran.

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com