Asilimia 10 ya kura zahesabiwa upya Iran | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 29.06.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Asilimia 10 ya kura zahesabiwa upya Iran

Nchini Iran zoezi la kuhesabu baadhi ya kura limeanza hii leo katika wilaya 22 zilizoko jimboni Teheran pamoja na majimbo mengine.Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia utata uliozuka baada ya uchaguzi uliofanyika tarehe 12.

Wafuasi wa Moussavi waliokusanyika hapo jana

Wafuasi wa Moussavi waliokusanyika hapo janaWakati huohuo Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad ameamuru kuchunguzwa kwa kifo cha Neda Agah-Soltan aliyeuawa wakati wa maandamano ya kuyapinga matokeo ya uchaguzi.Upinzani nchini humo unashikilia kuwa uchaguzi huo unapaswa kurudiwa badala ya kuhesabu baadhi ya kura.


Baraza kuu la kisheria nchini Iran la Guardian limeridhia hatua ya kuhesabu asili mia 10 ya kura zote kufuatia utata uliozuka baada ya uchaguzi wa Juni 12.Kiongozi wa upinzani Mir Hossein Moussavi ameipinga hatua hiyo na kushikilia kuwa uchaguzi mzima unapaswa kurejelewa.

Kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha televisheni cha taifa kura zimeanza kuhesabiwa tena katika wilaya 22 za Teheran pamoja na majimbo mengine nchini humo.Shirika rasmi la habari la kitaifa la IRNA limeeleza kuwa shughuli hiyo tayari imeshaanza katika jimbo la magharibi la Kurdistan.Zoezi hilo pia linaendelea na kusimamiwa na maafisa wa eneo hilo wa ngazi za juu katika mji wa Karaj ulio magharibi mwa Tehran kama lilivyothibitisha shirika la habari la Mehr.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa siku moja baada ya uchaguzi wa Juni 12 Rais Mahmoud Ahmedinejad ndiye aliyeibuka mshindi wa kura nyingi jambo lililosababisha maandamano yaliyodumu kwa kipindi cha siku kadhaa.Maandamano hayo yaliandaliwa na wafuasi wa mgombea wa upinzani Mir Hossein Moussavi anayedai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na hila.


Britische Botschaft in Teheran

Nje ya Ubalozi wa Uingereza mjini Teheran

Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa wafanyakazi wa ubalozi wa Uingereza nchini Iran wameachiwa baada ya kukamatwa kwasababu ya madai ya kuyachochea maandamano ya kuyapinga matokeo ya uchaguzi wa rais.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya mambo ya kigeni ya Iran Hassan Ghashghavi watano kati ya wafanyakazi wote tisa ndiwo walioachiwa.Iran kwa upande wake imekuwa ikiyalaumu mataifa ya magharibi hususan Uingereza na Marekani kuwa zinaingilia mambo yake ya ndani na kuyachochea maandamano.Waziri wa mambo ya Nje wa Uingereza David Milliband alisisitiza kuwa mawazo hayo ni potofu ''Wazo kwamba ubalozi wa Uingereza uliyachochea maandamano yaliyotokea Teheran katika kipindi cha majuma machache yaliyopita halina msingi.''


Hata hivyo Iran imetangaza kuwa haina mpango wowote wa kuzifunga balozi za mataifa hayo ya kigeni wala kusitisha uhusuiano wa kidiplomasia.Mataifa ya Umoja wa Ulaya nayo yamesisitiza kuwa endapo yatalazimika yatatoa kauli mwafaka ili kupambana na vitisho hivyo.

Wakati huohuo Rais Mahmoud Ahmedinejad ameamuru uchunguzi kufanywa ili kubaini chanzo cha kifo cha Neda Agah-Soltan aliyeuawa wakati wa maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi.Katika barua yake aliyomuandikia jaji mkuu Ayatollah Mahmoud Hashemi Shahroudi Rais Ahmedinejad ameiamuru hatua hiyo kwasababu ukweli haujabainika na huenda kisa hicho kitatumiwa na maadui kuiharibu sifa ya Iran.


Kwa upande mwengine mgombea wa urais wa upinzani aliyeshindwa Mir Hossein Moussavi amekutana na wanachama wa kamati maalum iliyoundwa kwa lengo la kuyachunguza matokeo ya uchaguzi huo uliogubikwa na utata.Bwana Moussavi anatarajiwa kuiwasilishia mapendekezo mapya kuhusu suala hilo.Kwa mujibu wa msemaji mmoja wa Baraza kuu la kisheria la Iran Abbasali Kadkhodai,Moussavi alikutana na wawakilishi wa kamati hiyo jana jioni na anatarajiwa kuyawasilisha mapendekezo yake hii leo.Hata hivyo maelezo kuhusu ufafanuzi wa mapendekezo hayo badao hayajafahamika.

Baraza kuu la kisheria la Iran la Guardian linatarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho baadaye hii leo na bado linasisitiza kuwa uchaguzi haukuwa na dosari zozote kubwa.


Takwimu za vyombo vya habari vya serikali zinaonyesha kuwa watu 20 waliuawa katika ghasia zilizotokea baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.Mvutano huo kati ya serikali na wafuasi wa upinzani umeitumbukiza Iran katika mkwamo wa kisiasa ambao ulishuhudiwa kwa mara ya mwisho wakati wa mapinduzi ya kiislamu yaliyotokea mwaka 1979.


Mwandishi:Thelma Mwadzaya AFPE/RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com