Ancelotti apuuza "kelele za Neymar"
27 Machi 2026
Ancelotti alisema wachezaji waliopo kwa sasa ndio wanaostahili kuzungumziwa.
Aliyasema haya baada ya Brazil kufungwa 2-1 na Ufaransa katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Alhamis huko Massachusetts Marekani, ambapo mashabiki wa Brazil baada ya mechi hiyo walisikika wakiimba jina la Neymar, wakiashiria kutaka kurudishwa kikosini kwa nyota huyo ambaye anasakata kandanda la klabu nchini Brazil kwa sasa.
"Kwa sasa tunastahili kuwazungumzia wale waliopo hapa, waliocheza, waliojitolea, waliojituma sana na nimeridhika," alisema Ancelotti.
Neymar, ambaye ndiye mfungaji bora wa Brazil akiwa na jumla ya mabao 79, hajaichezea Brazil tangu apate jeraha baya la goti mnamo Oktoba 2023 na hajacheza mara kwa mara katika klabu yake ya Santos aliyojiunga nayo mwaka jana.
Katika mechi hiyo ya kirafiki ya Alhamis, Ufaransa ilifungiwa mabao yake na Kylian Mbappe na Hugo Ekitike kisha Brazil ikapata la kufutia jasho kupitia kwa Bremer.
Miamba hao wa Amerika kusini watakuwa wanacheza na Croatia katika mechi ijayo ya kirafiki siku ya Jumanne kama sehemu ya kuiweka tayari kwa Kombe la Dunia litakaloanza mwezi Juni huko Marekani, Mexico na Canada.