1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amani Mashariki ya Kati

16 Oktoba 2010

Marekani inashutumu mpango wa ujenzi wa makaazi wa Israeli.

https://p.dw.com/p/PfWx
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Philip J. Crowley.Picha: cc-by-nd/Ralph Alswang

Serikali ya Marekani imeituhumu Israel kuwa mpango wake mpya wa kujenga zaidi ya makaazi 200 katika Jerusalem ya mashariki unahatarisha mchakato wa amani katika Mashariki ya Kati. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Philip Crowley amelalamika kuwa mpango huo unakwenda kinyume na jitahada za kuendeleza mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Amesema Marekani itaendelea kutafuta njia ya kuanzisha tena majadiliano hayo ya ana kwa ana. Safari hii Israeli iliiarifu Marekani  kuhusu ujenzi huo tofauti na ilivyokuwa mara ya mwisho. Wakati huo  habari za ujenzi mpya wa makaazi hayo zilitoka, pale makamu wa rais wa Marekani Joe Biden alipokuwa ziarani nchini humo kushinikiza mazungumzo ya amani. Hata hivyo Crowley hakusema iwapo mjumbe wa Marekani George Mitchell ana mipango ya kurejea katika Mashariki ya Kati.

Benjamin Netanyahu vor dem Untersuchungssausschus
Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Licha ya kukosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa,Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameidhinisha ujenzi wa kiasi ya nyumba mpya 240 katika eneo la Waarabu mashariki ya Jerusalem. Mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Saeb Erakat  amesema, Israeli ndio ya kulaumiwa kwa kuvunjika kwa mazungumzo ya amani.

Mwandishi: Maryam Abdalla/DPAE

Mpitiaji: Martin,Prema