Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 06.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani yaandika juu ya madai kwamba Majenerali wa Nigeria wanashirikiana na magaidi wa Boko Haram ,juu ya vijana wa Eritrea na ripoti ya Shirika la misaada la Ujerumani

Majenerali wa Nigeria watuhumiwa kushirikiana na Boko Haram

Majenerali wa Nigeria watuhumiwa kushirikiana na Boko Haram

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya madai kwamba Majenerali wa Nigeria wanashirikiana na magaidi wa Boko Haram. Gazeti hilo linasema kwamba haujawahi kutokea uzushi mkubwa kama huo nchini Nigeria. Lakini tokea kutekwa nyara wasichana zaidi ya mia tatu na magaidi wa Boko Haram ,pamezuka madai kwamba baadhi ya Majenerali wa jeshi la Nigeria wana uhusiano na kundi la magaidi wa Boko Haram.

Gazeti la "die tageszeitung" limeikariri taarifa ya gazeti moja la nchini Nigeria,"The Leadership" inayofahamisha kwamba Majenerali na maafisa wa ngazi za juu wamepatikana na hatia mbele ya mahakama ya kijeshi ya kuwapa Boko Haram silaha na habari.Wanajeshi hao bado hawajahukumiwa.Hata hivyo makao makuu ya jeshi la Nigeria yamesisitiza kwamba taarifa hiyo siyo ya kweli.

Marufuku kuwaunga mkono wasichana waliotekwa nyara

Gazeti la "Süddeutsche" pia limeandika juu ya Boko Haram lakini kwa kuuangalia msimamo wa serikali juu ya watu wanaofanya kampeni ya kutaka wasichana waliotekwa nyara waachiwe.

Gazeti hilo linaeleza kwamba serikali ya Nigeria inajaribu kuwanyamazisha wote wale wanaofanya kampeni ya kuwania kuwakomboa watoto waliotekwa nyara tokea mwezi wa Aprili. Mkuu wa polisi sasa ameyapiga marukufu maandamano au mikutano yote inayohusu kutekwa nyara kwa wasichana hao kwa madai kwamba kampeni hiyo inaweza kuzivuruga juhudi za serikali za kuwakabili magaidi wa Boko Haram.

Eritrea: vijana wakimbia

Gazeti la "der Freitag" limechapisha taarifa inayosema kwamba maalfu ya vijana wanaikimbia nchi yao kila mwezi. Sababu ni kwamba wanalazimishwa kulitumikia jeshi. Lakini gazeti hilo linaarifu kuwa njia wanazozitumia vijana hao ili kufika wanakokimbilia aghalabu huwa ni za hatari kubwa.

Gazeti la "Der Freitag" linasema kulingana na makisio ya Umoja wa Mataifa vijana wa Eritrea 40,000 wanaamua kuikimbia nchi yao kila mwezi ili kuepuka kulitumikia jeshi. Wengi wao hukimbilia,kwanza katika nchi jirani ya Ethiopia.Baada ya hapo wanaendelea na safari ya kuenda Uswisi au Sweden. Lakini gazeti la "der Freitag" linauliza jee ni nani anaefanikiwa kufika salama katika nchi hizo?.

Gazeti linasema kutokana na njia ya hatari ya baharini wanayoitumia vijana hao ,wengi wanafikwa na maafa.Vijana wa Eritrea wanaoikimbia nchi yao ni miongoni mwa wakimbizi wengi wanaokufa baharini. Gazeti la "der Freitag " linafahamisha kwamba muda wa kulitumikia jeshi nchini Eritrea hauna mwisho kwa vijana wa nchi hiyo.

Sababu ya vijana hao kulazimishwa kulitumikia jeshi

Kuanzia mwaka 1998 na 2001 yametokea mapigano baina ya Eritrea na Ethiopia kutokana na mgogoro wa mpaka. Rais wa nchi hiyo Isayas Afewerki anautumia mgogoro huo ili kuyaimarisha mamlaka yake.

Bora kuekeza kuliko kutoa misaada ya dharura
Gazeti la "Berliner Zeitung" limeichapisha ripoti ya mwaka wa 2013 ya Shirika la Ujerumani linalotoa misaada ya chakula duniani."Welthungerhilfe" Gazeti hilo limemnukuu Katibu Mkuu wa Shirika hilo bwana Wolfgang Jamann akisema kwamba idadi ya maafa makubwa yanayowakumba binadamu imeongezeka duniani kutokana na migogoro ya kivita. Maafa yamefikia kiwango cha kutisha. Kutokana na hali hiyo watu zaidi na zaidi wanaitegemea misaada ya dharura.

Gazeti la "Berliner Zeitung" limemnukuu Katibu Mkuu huyo akieleza kwamba fedha nyingi zinatumika kwa ajili ya kutoa misaada ya dharura badala ya kuziekeza katika miradi ya maendeleo ya muda mrefu.Ripoti ya Shirika la Ujerumani la misaada ya chakula imetoa mfano wa hali ya nchini Sudan Kusini. Ripoti imesema kuwa hakuna njia nyingine ya kuiepuka hali hiyo ila kuleta amani katika nchi hiyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman