Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 03.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya biashara ya pembe za ndovu na juu ya mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi wa Mali yanayotolewa na wakufunzi wa Ujerumani.

Bishara ya pembe za ndovu yastawi Afrika

Biashara ya pembe za ndovu yastawi Afrika

Wiki hii pia,gazeti la "Bild am Sonntag"linatufahamisha juu ya nguo za hisani zinazotolewa nchini Ujerumani kwa ajili ya kuwasaidia watu barani Afrika .Jee nguo hizo zinaenda wapi?

Wanajeshi wabaka wanawake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wametoa madai mazito dhidi ya kampuni ya mbao inayoitwa Danzer ya Ujerumani na Uswisi. Gazeti la"die tageszeitung" limeripoti kwamba wanajeshi waliokuwamo katika lori la kampuni hiyo waliwawavamia raia katika kijiji cha Bongulu.

Gazeti hilo linatufahamisha zaidi kwamba katika usiku wa kuamkia tarehe 2 wanajeshi wapatao sitini pamoja na polisi walikivamia kijiji cha Bongulu katika sehemu ya Yakilisa. Wanajeshi na polisi hao walikuwamo ndani ya Lori la kampuni ya mbao ya Ujerumani na Uswisi inayoitwa Danzer.

Gazeti la"die tageszeitung" limeandika katika taarifa yake kwamba wanajeshi na polisi hao waliwabaka wanawake sita na pia waliwakamata wanaume 16. Askari hao waliwapakia watu hao 16 katika lori la kampuni nyingine inayoitwa Siforco na kuondoka nao.Kwa mujibu wa gazeti la "die tageszeitung" watu hao waliteswa njiani. Na walipofika katika sehemu inayoitwa Engengele,wanajeshi na polisi waliwakabidhi wanaume hao 16 kwa meneja wa kampuni,anaeitwa Klaus Hansen mwenye nasaba ya Denmark.

Wanajeshi wahongwa?

Wanajeshi walipewa bahasha iliyojaa kitita cha manoti, na meneja huyo.Madai hayo yametolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya ECCHR na Global Witness.Lakini kampuni za mbao za Danzer na Siforco, zote za Ulaya, zimeyakanusha madai hayo.

Pembe za ndovu
Gazeti la" NZZ am Sonntag" limechapisha makala juu ya biashara ya pembe za ndovu.Gazeti hilo linasema kwamba biashara hiyo imezidi kustawi barani Afrika .

Pembe za ndovu zinaingizwa barani Ulaya pia kinyume cha sheria .Na sasa watafiti wanapiga mbiu ya mgambo. Gazeti hilo linaarifu kwamba theluthi mbili ya ndovu wameshaangamia tokea mwaka 2002 barani Afrika .Ingawa biashara ya pembe za ndovu imepigwa marufuku,bado inaendelea kustawi.Wanunuzi wakuu ni China na Thailand. Gazeti la "NZZ am Sonntag" limeinukuu ripoti ya mashirika ya ulinzi wa wanyamapori inayosema kuwa biashara haramu ya pembe za ndovu imeongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Mafunzo kwa wanajeshi wa Mali,yamechelewa?

Gazeti la"die tageszeitung"wiki hii pia limendika juu ya mgororo wa nchini Mali. Limeripoti juu ya mafunzo yanayotolewa na wanajeshi wa Ujerumani kwa askari wa nchi hiyo.Gazeti hilo limearifu kwamba mafunzo hayo maalumu yanatolewa kwanza kwa askari 30. Askari hao watapewa mafunzo juu ya kuzuia barabara, kumdhibiti adui,na njia za kuwahudumia majeruhi.Lakini Gazeti hilo limewanukuu wataalamu wakisema kuwa mafunzo hayo yamechelewa.


Jee nguo za msaada zinazotolewa na Wajerumani zinaenda wapi?

Ripota wa gazeti la "Bild am Sonntag" Thilo Mischke analijibu swali hilo katika taarifa yake. Ripota huyo alienda Nairobi na kufanya kazi kwenye soko la mitumba la Gikomba jijini Nairobi.

Anaeleza kwamba Wajerumani wanatoa nguo thamani ya Euro Bilioni moja na nusu kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji.Nguo hizo zinazotolewa kwa hisani na Wajerumani zinafanyiwa biashara .Mwandishi huyo,Thilo Mischke anasema katika taarifa yake kwamba, siyo Waafrika peke yao wanaonufaika na biashara hiyo.Kampuni moja inayoitwa Soex iliyopo katika mji wa Bad Oldesloe nchini Ujerumani,iliuza tani 85,000 za mitumba na kuingiza kiasi cha Euro Milioni 58 mnamo mwaka wa 2010.


Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman