1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya14 Januari 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya juhudi za Umoja wa Afrika katika kuzipatanisha nchi mbili za Sudan,mgororo wa Mali na mazingira ya mashaka yanayowakabili mashoga katika nchi nyingi za Afrika

https://p.dw.com/p/17JJg
Wanajeshi wa Ufaransa tayari wapo Mali kulisaidia jeshi la nchi hiyo
Wanajeshi wa Ufaransa tayari wapo Mali kulisaidia jeshi la nchi hiyoPicha: REUTERS/ECPAD/Adj. Nicolas Richard/Handout

Gazeti la"Berliner Zeitung"linazungumzia juhudi za Umoja wa Afrika katika kujaribu kuzipatanisha nchi mbili za Sudan.

Limeandika kuwa Marais wa Sudan ya Kusini Salva Kirr na Omar Bashir wa Sudan walipeana mikono bila ya kuambiana neno hata moja.Gazeti la"Berliner Zeitung" limemkariri mpatanishi wa Umoja wa Afrika Thabo Mbeki akisema kuwa kwenye mpaka wa kilometa karibu 2000 taratibu za amani zinapaswa kuwekwa.Taratibu hizo ni pamoja na kuyaondoa majeshi kwenye mpaka huo.

Gazeti la"Berliner Zeitung"linasema katika makala yake kwamba nchi mbili za Sudan zimo katika mtanziko wa kujiteketeza.Kwani nchi hizo zinategemea sana mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta.Wakati mafuta yapo Sudan ya Kusini,mabomba ya kuyasafirishia mafuta hayo yapo kaskazini.Gazeti la"Berliner Zeitung"linasema sasa ni juu ya msuluhishi wa Umoja wa Afrika, Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki kufanya juhudi za kuleta amani baina ya nchi mbili za Sudan. 

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine"wiki hii limechapisha taarifa juu ya mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Katika taarifa hiyo gazeti hilo linafahamisha kuwa waasi wa M23 wameamua kwa upande wao kusimamisha mapigano,siku chache kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo baina yao na wajumbe wa serikali. Katibu Mkuu wa M23 Francois Rucogoza amesema waasi wataendelea kunyamazisha silaha katika upande wao hata ikiwa upande wa serikali hautakubaliana na hatua hiyo. 

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine"limetilia maanani katika taarifa yake kwamba serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mpaka sasa inalikataa pendekezo la kuzinyamazisha silaha.Gazeti hilo pia limeripoti kwamba matayarisho yanaendelea ya kuyapeleka majeshi ya nchi za Afrika kuingilia kati katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Nchi za maziwa makuu ziliamua kwenye mkutano wa mjini Addis Ababa kupeleka jumla ya askari 4000 nchini Kongo.


Gazeti la "die tageszeitung" limechapisha makala inayozungumzia mgogoro wa nchini Mali.Linasema Mali imesimama kati ya mapigano na mazungumzo.Wakati juhudi za kuleta suluhisho zinaendelea madola ya Nato yametolewa mwito wa kusaidia kijeshi. Licha ya hatua za kijeshi,suluhisho la amani linandelea kutafutwa. Na gazeti la "der Freitag" linasema katika taarifa yake kuwa Algeria na Burkina Faso zilijaribu kusuluhisha katika mgogoro wa Mali.

Mashoga:

Katika nchi nyingi za Afrika mashoga wanaandamwa na wakati mwingine maisha yao yanatishiwa. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la"Süddeutsche Zeitung" Gazeti hilo linaarifu juu ya mkasa wa baba mmoja,kwa jina Mbede nchini Kamerun. Gazeti la"Süddeutsche linaarifu kuwa baba huyo Jean Claude Roger Mbede alituma ujumbe wa simu kumwambia mtu mwengine "nakupenda."

Alieupokea ujumbe huo alikuwa mwanamume mwenzake.Kwa ujumbe huo,Mbede alijichongea.Gazeti la "Suddeutsche limefahanisha kwamba Mbede alikamatwa na kufungwa jela.Mkasa huo umetokea nchini Kamerun ambako kuna sheria  inayopiga marufu ushoga.Katika nchi nyingi barani Afrika ushoga ni kosa na katika nchi kama Sudan adhabu yake inaweza kuwa kifo.

katika nchi hizo ushoga unazingtiwa kuwa ni kinyume cha maadili na pia ni kinyume cha uafrika.Kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 347,mtu anaweza kupewa adhabu ya kifungo jela cha hadi miaka mitano ikiwa anapatikana na hatia ya matendo ya ushoga nchini Kamerun.Gazeti la Südeutsche "linasema mazingira hayo magumu yanawakabili mashoga katika takriban theluthi mbili ya nchi za Afrika.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri:Mohammed Khelef