Adhabu ya kifo inapingwa | Masuala ya Jamii | DW | 01.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Adhabu ya kifo inapingwa

Mkutanowa kimataifa umeanza leo katika mji huu mkuu wa Ufaransa, ambapo wajumbe zaidi ya elfu moja wanazungumzia mikakati ya kuiondoa adhabu ya kifo. Bado nchi 70 duniani zinatumia adhabu hiyo.

Nchini Marekani kunatumika sidano za sumu

Nchini Marekani kunatumika sidano za sumu

Ufalme wa Toskana nchini Italia ni taifa la kwanza duniani, ambalo liliondoa adhabu ya kifo, mwaka 1789. Miaka 160 baada ya hapo, vita vya pili vya dunia vilipomalizika, kwa jumla mataifa kumi tu yaliondoa adhabu hiyo, ikiwemo pia Ujerumani ya Magharibi.

Leo hii zaidi ya nusu ya mataifa yote 200 duniani yamebatilisha adhabu ya kifo ikiwa ni kwa sheria au kwa kutoitumia tena. Tena idadi hiyo inazidi kuongezeka.

Anayefurahi juu ya mwenendo huu ni Robert Badinter, waziri wa zamani wa sheria wa Ufaransa ambaye kama waziri aliondosha adhabu ya kifo nchini humu mwaka 1981. Alisema: “Wakati huo sikuamini kuwa baada ya miaka 25, zaidi ya nusu ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zitaondosha adhabu ya kifo. Na hata kuwa kwenye bara zima la Ulaya, adhabu hiyo haitumiki tena. Huo ni ushindi mkubwa kwetu na ni ushindi ambao haukutarajiwa.”

Lakini bado adhabu hiyo inatumika katika nchi nyingi. Mwaka wa 2005 watu 2100 wanajulikana kuuawa kutokana na kuadhibiwa kifo, sehemu kubwa kati yao waliuawa nchini China, Saudi Arabia, Iran na Marekani. Kwa hivo, Marekani ni moja kati ya nchi chacha za kidemokrasi ambazo bado zinaendesha adhabu ya kifo.

Katika baadhi ya nchi adhabu ya kifo haitumiki tu katika kesi za matumizi ya nguvu, bali pia katika maeneo mengine ya kisheria. Mfano Saudi-Arabia ambapo vitendo vya kishoga huadhibiwa kifo, nchini Cuba ni katika kesi za rushwa, katika Umoja wa Falme za Kiarabu ni kwa vitendo vya kuharibu mazingira na katika maeneo fulani ya Uchina watu wamepewa adhabu ya kifo baada ya kufanya wizi mdogo wa unyakuzi.

Kulingana na sheria ya kimataifa hairuhusiwi kuwapa watoto na vijana ambao hawajafika umri wa miaka 18 adhabu ya kifo. Hata hivyo, kuna nchi kadhaa ambazo huwaua watoto na vijana, ambazo ni Nigeria, Saudi-Arabia, Pakistan, Iran na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Lengo la mkutano huu wa Paris unaoendelea hadi Jumamosi ni kuzungumzia njia za kupiga vita kutolewa hukumu za adhabu ya kifo. Wanaohudhuria ni wajumbe wa shughuli za siasa, makanisa, mawakili, mashirika ya kutetea haki za binadamu na jamaa watu walioathirika. Kwenye warsha na semina zao, wajumbe hawa wanataka kutafuta mikakati ya kidiplomasia, kwa mfano katika kuishurutisha Uchina kupunguza idadi ya adhabu za kifo. Huenda mashindano ya kimataifa ya Olympiki yatakaofanyika Uchina mwaka ujao yanapaswa kutumika kama jukwaa la kuilazimisha Uchina, kwani wakati huo dunia nzima itaiangalia Uchina.

Wanaharakati hawa tayari wanahisi kama wako njiani kufika lengo la kubatilisha adhabu ya kifo, kwani siku hizi ni wale wanaoitumia adhabu hiyo ambao wanalazimika kujitetea na siyo tena wapinzani wa adhabu hiyo.

 • Tarehe 01.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlg
 • Tarehe 01.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlg
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com