Zimbabwe: Kampeni ya duru ya pili ya uchaguzi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 26.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Zimbabwe: Kampeni ya duru ya pili ya uchaguzi

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amezianza kampeni zake kwa ajili ya duru ya pili ya tarehe 27 mweji ujao akitishia hata kumtimua balozi wa Marekani nchini mwake kwa tuhuma za kuingilia kati maswala ya ndani ya Zimbabwe.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe


Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amezianza kampeni zake kwa ajili ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais tarehe 27 mweji ujao akitishia hata kumfukuza balozi wa Marekani nchini mwake kwa tuhuma za kuhusika na maswala ya ndani ya Zimbabwe.


Katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni mpya ya uchaguzi kwa ajili ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais mbele ya mashabiki kiasi ya 2000 katika mji mkuu wa Zimbabwe Harare, jana rais Robert Mugabe alisema atakubali matokeo ya uchaguzi ila wafuasi wake wajitayarishe kuutetea kwa kila hali uhuru wa taifa ikibidi wafe. Rais Mugabe alizishutumu kwa mara nyingine tena mkoloni wa zamani Uingereza na Marekani kwamba nchi hizo za magharibi zinajiingiza katika mambo ya ndani ya Zimbabwe. Hasa rais Mugabe alitishia kumfukuza balozi wa Marekani James McGee ikiwa ataendelea kufanya namna anavyokuwa akifanya sasa hivi. Rais Mugabe alimshutumu balozi McGee kwamba amekuwa akishirikiana na upinzani unaoongozwa na Morgan Tsvangirai akisema " siku balozi McGee alimuita Morgan hebu rudi nyumbani, alifanya hivyo akiruka". Hapo rais Mugabe alikuwa akimaanisha wakati Morgan Tsvangirai alikuwa nje ya nchi akiogoka hata kurudi nyumbani akihofia usalama wake. Marekani imeyatafsiri matamshi hayo ya rais Mugabe kuwa ni kitisho cha kumnyanyasa balozi wake nchini Zimbabwe.

Kwa upande wake kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai, ameianza kampeni ya uchaguzi kwa kuwatembelea wahanga wa machafuko ya kisiasa wanaolazwa katika hospitali ambao alisema wamebaki majasiri tu:


" Leo nimekuwa katika hospitali. Watu wakiwa na kovu na wengine wakiwa na majiraha, wamesema wote kwa pamoja, rais tutammaliza, tusiregeze kamba. Kwa hiyo ujasiri wa hao watu ambao licha ya kukabiliwa na usumbufu wako tayari kuendelea mpaka mwisho ni jambo limenitia moyo"


Rais Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 84 sasa na ambae anaitawala Zimbabwe tangu uhuru mwaka wa 1980, anazilaumu pia nchi za magharibi kusababisha uchumi wa taifa lake kuzidi kuporomoka. Mfumko wa bei umezidi kuvunja rikodi na kufikia sasa zaidi ya asili mia 165 elfu. Asili mia 80 ya watu hawana kazi na chakula na mafuta vimezidi kukosekana. Hali hiyo ngumu kimaisha ndiyo ilikuwa imesababisha raia wengine kiasi ya milioni 3 na nusu kuhamia nchini Afrika ya kusini lakini baadhi yao wamelazimika kurudi nyumbani kutokana na mashambulizi ya hivi karibuni ya wenyeji dhidi ya raia wa kigeni.

Rais Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF wanategemea kura zaidi sehemu za vijijini huku mpinzani wake Morgan Tsvangirai akitegemea zaidi kura za mijini.

Ni katika mazingira hayo wanasiasa hao wawili hasimu wanajiandaa kuchuana tarehe 27 juni kuamua ni nani atakayeitawala Zimbabwe kwa muhula ujao.

 • Tarehe 26.05.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E69X
 • Tarehe 26.05.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E69X
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com