Ziara ya kansela Angela Merkel barani Afrika magazetini wiki hii | Magazetini | DW | 14.10.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ziara ya kansela Angela Merkel barani Afrika magazetini wiki hii

Ziara ya kansela wa Ujerumani barani Afrika ndio mada iliyogonga vichwa vya habari .Hata hivyo azma ya Burundi kujitoa katika korti kuu ya kimataifa ya Uhalifu ICC sawa na onyo la Marekani kwa DRC hazikusahauliwa

Bendera ya Ujerumani yapepea kansela Merkel alipokuwa ziarani Afrika

Bendera ya Ujerumani yapepea kansela Merkel alipokuwa ziarani Afrika

 

Tunaanza lakini na ziara ya kansela  Angela Merkel nchini Mali,Niger na Ethiopia. Kote huko mada kuu ilihusiana na juhudi za kuzisaidia nchi hizo kuinua maendeleo pamoja na kukabiliana na wimbi la wakimbizi wanaoyatosa maisha yao baharini kwa tamaa ya kuja Ulaya.

Gazeti la die Tageszeitung linaichambua ziara hiyo katika ripoti iliyopewa kichwa cha maneno "ziara ya kasi barani Afrika."Siku tatu,nchi tatu,ziara hiyo ya Angela Merkel imelengwa kujaribu kuzijua sababu zinazowafanya watu kuelekea Ulaya. ilikuwa ziara ya kujifunza, lengo bayana likiwa kupunguza mikururo ya wakimbizi- limeandika gazeti hilo la mjini Berlin.

Katika wakati ambapo serikali yake inakosolewa vikali kutokana na sera yake kuelekea wakimbizi,Angela Merkel ametaka kujionea mwenyewe,kule kule wakimbizi wanakotokea,kipi hasa kinawafanya watu wakimbilie Ujerumani. Kupambana na sababu za hali hiyo ni njia mojawapo ya kuudhibiti mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya,hayo kansela Merkel amekuwa akiyasema tangu mwaka mmoja uliopita,kila wakati fursa inapojitokeza.

Lakini hilo linamaanisha nini na nini kinachowafanya watu hao wasalie nchini mwao linajiuliza gazeti la die Tageszeitung? Gazeti la Die Zeit limechapisha mahojiano waliyokuwa nayo na kansela Merkel kabla ya ziara yake barani Afrika. Katika mahojiano hayo kansela Merkel amezungumzia mkakati mpya wa sera za Umoja wa Ulaya kuelekea bara  jirani la Afrika.

Ripoti ya makubaliano ya Malta kuchapishwa mapema mwaka 2017

Katika mahojiano hayo pamoja na gazeti la Die Zeit kansela Merkel amesema ni kwa masilahi ya Ujerumani kuhakikisha hali ya maisha ni nzuri barani Afrika."Anaetaka kuwazuwia watu wasiyape kisogo maskani yao,anabidi ahakikishe katika nchi zao wanaishi katika hali inayostahiki." alisema kansela Merkel katika mahojiano hayo pamoja na gazeti la Die Zeit lililokumbusha makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mkutano kati ya viongozi wa Umoja wa ulaya na wale wa Afrika,mkutano uliofanyika Novemba 12 mwaka 2015 katika kisiwa cha Malta kilicho katika Bahari ya Mediterania.

Makubaliano hayo yanazungumzia kuhusu kuundwa fuko maalum kugharimia miradi itakayopelekea kupunguzwa wimbi la wahamiaji kinyume na sheria. Ripoti ya kwanza inayotathmini yaliyofikiwa itachapishwa mapema mwakani,linamaliza kuandika gazeti la Die Zeit.

Gazeti la Die Welt linazungumzia pia mzozo wa wakimbizi lakini kwa kufungamanisha na faharasa iliyochapishwa wiki hii kuhusu hali ya njaa ulimwenguni. Die Welt linasema katika zile nchi masikini kabisa za dunia,hakuna mkimbizi anaekuja Ulaya. Gazeti linaitaja jamhuri ya Afrika kati inayoburura mkia katika faharasa hiyo kwa mwaka 2016.

Burundi yapanga kujitoa katika ICC

Burundi kujitoa katika korti ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague ni mada iliyoripotiwa na gazeti mashuhuri la Frankfurter Allgemeine. Gazeti hilo linasema bunge la Burundi limepiga kura kwa wingi mkubwa kujitoa katika Mkataba wa Roma unaoishurutisha Burundi kushirikiana na korti ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague. Ili uamuzi huo wa bunge uanze kufanya kazi,patahitajika wingi wa kura pia kutoka baraza la Senet,linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine linalohisi uamuzi huo utaidhinishwa tu. Kwa namna hiyo Burundi itakuwa nchi ya kwanza kufutilia mbali uwanachama wake katika korti ya ICC. Chanzo cha hayo linaendelea kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine ni kuvunjwa  vibaya sana haki za binaadam nchini humo. Linamaliza kuandika gazeti la Frankfurter Allgemeine.

Kitisho cha kuzuka Vurugu katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusiana na onyo la Marekani dhidi ya kitisho cha kuzidi kuvurugika hali ya mambo katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Lilikuwa gazeti la die Tageszeitung lililomnukuu mjumbe maalum wa Marekani katika eneo la maziwa makuu Tom Perriello akisema jumuia ya kimataifa inabidi imshinikize rais Kabila ili uchaguzi uitishwe kama ilivyopangwa ili kuepusha balaa la machafuko.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE

Mhariri: Daniel Gakuba