1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 120 wauwawa kwenye ghasia nchini Kenya

Josephat Charo31 Desemba 2007

Waandamanaji wapinga vikali ushindi wa rais Mwai Kibaki dhidi ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga

https://p.dw.com/p/CiWm
Polisi wakimtia mbaroni mkenya huyu katika mtaa wa mabanda wa Kibera jijini NairobiPicha: AP

Ghasia na machafuko yanayoendelea kote nchini Kenya yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 124. Taarifa hiyo imetangazwa na televisheni ya KTN hii leo mjini Nairobi.

Polisi nchini Kenya wamekabiliana na waandamanaji mjini Nairobi, kufuatia hatua ya tume huru ya uchaguzi kumtangaza mgombea wa chama cha PNU, rais Mwai Kibaki, kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika nchini humo Alhamisi iliyopita.

Maandamano makubwa yamefanyika kuanzia eneo la magharibi karibu na mpaka wa Kenya na Uganda, hadi katika mitaa ya madongo poromoka ya mjini Nairobi. Machafuko yameripotiwa pia katika mji wa Mombasa katika mkoa wa pwani.

Kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa na shirika la habari la Reuters watu waliouwawa imefikia 70 lakini televisheni ya KTN imesema idadi hiyo imeongezeka na kufikia watu 124 hivi.

Katika mji wa Kisumu, ngome ya chama cha upinzani cha ODM, maiti 21 zilizopelekwa katika hospitali moja mjini humo wakati wa usiku na leo asubuhi, zimeonekana zimezagaa katika chumba cha kuhifadhia maiti. Nyingi ya maiti hizo zilikuwa na majeraha ya risasi.

Wakati huo huo, kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, ameitisha maandamano ya amani kupinga ushindi wa rais Mwai Kibaki. Kiongozi huyo amesema atakuwa kila mara akiwajulisha polisi juu ya hatua wanayotaka kuchukua lakini akasisitiza kutafanyika maandamano ya amani.

Kumekuwa na taarifa kwamba viongozi wa polisi wamewakamata baadhi ya viongozi wa chama cha ODM lakini msemaji wa serikali, bwana Alfred Mutua, amekanusha madai hayo.

Pia kumekuwa na tetesi kwamba kamanda wa polisi jenerali mstaafu Hussein amejiuzulu pamoja na kamanda mmoja wa jeshi lakini bwana Mutua pia amekunusha taarifa hizo.

Sambamba na hayo, Marekani imesema leo kwamba ina wasiwasi juu ya matatizo yaliyotokea wakati wa zoezi la kuhesabu kura na kuwataka viongozi wajizuie wasifanye machafuko.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa Marekani mjini Nairobi imesema wale wanaodai kumekuwa na mizengwe wanatakiwa wawasilishe malalamiko yao mahakamani na kutumia sheria inayoruhusu uhuru wa kujieleza, wataweza kuitangaza kesi yao hadharani. Taarifa hiyo pia imeitaka mahakama nchini Kenya itimize jukumu lake kwa njia ya haki.

Habari za hivi punde zinasema rais Kibaki ameahidi kuimarisha usalama kote nchini katika ujumbe wake wa mwaka mpya.