1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa wajeruhiwa katika sherehe za carnival

25 Februari 2020

Watu kadhaa wamejeruhiwa baada ya mtu aliyekuwa akiendesha gari kuuvamia umati wa watu waliokuwa wakisherehekea tamasha la Carnival Ujerumani. Polisi wamemkamata mshukiwa na wamesema ni tukio la makususdi.

https://p.dw.com/p/3YMV4
Deutschland Auto fährt in Karnevalsumzug in Hessen
Picha: picture-alliance/dpa/S. Pförtner

Watu 30 wamejeruhiwa hapo jana ikiwa ni pamoja na watoto katika mji mdogo wa Volkmarsen magharibi mwa Ujerumani, baada ya raia wa Kijerumani aliyekuwa ndani ya gari kulivamia gwaride la watu waliokuwa wakisherehekea tamasha la kitamaduni la 'Karnival'.

"Alikuwa akiliendesha gari kwa kasi kuelekea kwenye umati wa watu. Hisia yangu ni kwamba alikuwa akiongeza kasi. Kulikuwa na sekunde chache za ukimya halafu kila mtu akaanza kupiga kelele," amesema Friedhelm Engelmann, mmoja wa wakazi walioshuhudia tukio hilo.

Waendesha mashtaka wa Ujerumani pamoja na polisi wamesema mshukiwa huyo, kijana mwenye umri wa miaka 29, amekamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuua. Wameongeza kwamba sababu bado haijulikani, lakini tukio hilo linazingatiwa kuwa ni la makusudi huku uchunguzi ukiwa unaendelea.

"Hatufikiri kuwa hili lilikuwa ni shambulio la kigaidi. Lakini linaweza kuzingatiwa kama shambulio la makusudi. Bado hatujui sababu zake. Mahojiano ya hadi sasa hayatoshi kuweza kusema chochote kuhusu nia ya shambulio hili," ameeleza msemaji wa polisi wa jimbo la Hesse, Henning Hinn.

Deutschland Auto fährt in Karnevalsumzug in Hessen
Gari laendeshwa kwenye gwaride la Carnival huko Hesse, Ujerumani Picha: picture-alliance/dpa/U. Zucchi

Wengi waliojeruhiwa ni watoto

Waziri wa ndani wa jimbo la Hesse, Peter Beuth, amesema thuluthi moja ya waliojeruhiwa ni watoto. Kati ya watu wanane hadi kumi miongoni mwa hao thelathini wamejeruhiwa vibaya sana.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya mtu mmoja kuwaua watu tisa kwa kuwapiga risasi kabla ya kumuua mama yake na yeye mwenyewe kujiua, katika moja ya mashambulio mabaya zaidi ya ubaguzi wa rangi kushuhudiwa Ujerumani tangu Vita vya vya Pili vya Dunia.

Soma zaidi:Ujerumani yakiri kitisho cha itikadi kali

Msemaji wa polisi na waendesha mashtaka wamekataa kutoa kauli yoyote juu ya taarifa za vyombo vya habari kwamba polisi imemkamata mshukiwa mwengine anaehusishwa na tukio hilo.

Mnamo mwaka 2016, raia mmoja wa Tunisia mwenye mafungamano na wanamgambo wenye misimamo mikali ya dini ya Kiislamu aliendesha gari na kuwagonga watu waliokuwa kwenye soko la Krismasi mjini Berlin, na kusababisha vifo vya watu 12. Baadae naye aliuliwa na maafisa wa polisi wa Italia baada ya kukimbia Ujerumani.

Vyanzo: (rtre,afpe)