Wakurdi wapambana na IS mjini Kobane | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wakurdi wapambana na IS mjini Kobane

Wanamgambo wa Dola la Kiislamu wanakaribia kuukamata mji muhimu wa Syria, Kobane, katika mpaka wa Uturuki, baada ya kuzitwaa wilaya tatu za mashariki mwa mji huo kufuatia makabiliano makali na wapiganaji wa Kikuurdi

Mji wa Kobane unaofahamika pia kama Ain al-Arab, umekuwa uwanja muhimu wa mapambano baina ya kundi la Dola la Kiislamu – IS na wapinzani wake, ambao ni pamoja na Marekani na washirika wake wa Magharibi na Kiarabu.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria, mapigano yamesambaa katika maeneo mapya ya kusini na magharibi ya mji wa Kobane. Kama kundi la IS litaweza kuuteka mji huo, basi litaudhibiti ukanda mrefu wa mpaka wa Syria na Uturuki. Wanajihadi hao wamefanya mashambulizi ya karibuni katika mji wa Kobane baada ya kuuzingira mji huo kwa wiki tatu, ikiwa ni pamoja na wimbi la mashambulizi ya mabomu ya kujitoa mhanga.

Baada ya kujipenyeza katika mji huo, wanamgambo hao walikabiliana vikali na wapiganaji wenyeji wa Kikurdi, ambao wameapa kupigana hadi dakika ya mwisho ili kujaribu kuukomboa. Mapigano hayo yamewalazimu mamia ya raia kukimbilia karibu na mpaka wa Uturuki. Wapiganaji wa Kikurdi wamewaamuru raia wote kuuhama mji huo.

Syrien Kobane Kämpfe Rauch Presse 05.10.2014

Raia wakishuhudia kwa umbali mapigano yanayoendelea Kobane, Kati ya IS na wapiganaji wa Kikurdi

Hayo yanajiri wakati mpiga picha wa shirika la habari la AFP akisema ameona bendera mbili nyeusi za kundi hilo la jihadi kipepea katika upande wa mashariki mwa mji wa Kobane. IS ilianza kuushambulia mji wa Kobane mnamo Septemba 16, ikilenga kuchukua udhibiti wa sehemu kubwa ya mpaka wa Syria na Uturuki. Hali hiyo ilisababisha karibu wau 186,000 kukimbilia Uturuki.

Hapo jana vikosi vya usalama vya Uturuki vilitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya raia na wanahabari waliokusanyika katika eneo hilo la mpakani kushuhudia makabiliano ya Kobane. Wiki iliyopita serikali ya Uturuki iliidhinisha serikali kujiunga na kampeni inayoongozwa na Marekani ya kupambana na IS, lakini kufikia sasa, hakuna mipango yoyote ya hatua ya kijeshi iliyotangazwa.

Uturuki imeviweka vifaru vyake katika eneo la mpakani karibu na mji wa Kobane, lakini haijawatuma wanajeshi wake kwenda kuwasaidia wapiganaji wa Kikurdi. Kiongozi mpya wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameapa kuilinda Uturuki ambayo ni mwanachama wake, dhidi ya shambulizi la IS.

Nchini Syria, jeshi la muungano likiongozwa na Marekani limeendelea kuyalipua maeneo ya IS karibu na Raqa, Deir Ezzor na Kobane. Pia mashambulizi yamefanywa karibu na miji ya Fallujah na Ramadi nchini Iraq, huku Ubelgiji na Uingeteza zikishiriki katika operesheni hiyo.

Helikopta za jeshi la Marekani zimeanza kufanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa IS, hali inayoashiria kuongezeka kwa vita vya angani ambavyo vinayaweka majeshi ya Marekani katika kitisho kikubwa.

Mwandishi: Bruce Amani / AFP
Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com