1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshikamano barani Ulaya

15 Oktoba 2015

Kansela Angela Merkel ameipinga fikra ya kufungwa mipaka ya Ulaya kutokana na wimbi la wakimbizi, akisema watu wanabidi wawe na mshikamano na kutoa wito wa kulindwa vyema zaidi mpaka kati ya Ugiriki na Uturuki.

https://p.dw.com/p/1Gp1H
Kansela Angela Merkel akilihutubia bunge la shirikisho -Bundestag,mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa/v. Jutrczenka

Matamshi hayo yametolewa na kansela Angela Merkel katika wakati ambapo viongozi wa Umoja wa ulaya wanakutana wakati huu tulio nao mjini Brussels kwa kikao maalum kitakachozungumzia miongoni mwa mengineyo, mzozo wa wakimbizi.

Akizungumza mbele ya wabunge wa Ujerumani mjini Berlin,kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa ulaya utakaozungumzia suala hilo hilo,magharibi ya leo mjini Brussels, kansela Angela Merkel amesema anahisi Umoja wa ulaya unabidi uisaidie Uturuki hasa kuilinda vyema mipaka yake kwasababu ujia wa bahari kati ya Uturuki na Ugiriki unadhibitiwa hivi sasa na maharamia wanaowaingiza watu kinyume cha sheria."

Kwa jumla,na kutokana na mzozo huu wa wakimbizi,panahitajika Ulaya ya mshikamano, njia yoyote nyengine haitofuzu" amesema kansela Merkel,katika wakati ambapo nchi za Ulaya ya Mashariki na hasa kule ambako wakimbizi wanapitia katika eneo la Balkan zimezidisha hatua za ukaguzi mnamo wiki za hivi karibuni.

Sera za kuifunga milango ya Ulaya haisaidii kitu

"Kufungwa mipaka ya Ulaya ni ndoto katika karne ya 21 ambayo ni karne ya mtandao" amesema kansela Merkel akijibu lawama anazotupiwa humu nchini hasa kutokana na siasa yake karimu kuelekea wakimbizi-siasa inayokosolewa mpaka ndani ya chama chake cha kihafidhina cha CDU na washirika wao wa CSU."Hatutii chunvi tukizungumzia kuhusu changamoto yenye kipeo cha kihistoria" kwa ulaya " ameongeza kusema kansela Merkel.

Angela Merkel Ankunft Brüssel Belgien EU Treffen Versammlung
Kansela Merkel awasili Brussels kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/dpa/S. Lecocq

Zaidi ya wakimbizi laki saba wameingia katika nchi za umoja wa ulaya kati ya januari mosi na septemba 30 mwaka huu-kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa mapema wiki hii na taasisi ya Umoja wa Ulaya ya kuchunguza mipaka-Frontex.Nchini Ujerumani tu,wakimbizi hadi milioni moja wanatazamiwa kuwasili mwaka huu na mzigo huo unadhihirika kupindukia uwezo wa mapokezi.

Ufumbuzi utapatikana kwa kuzidi kuisaidia Uturuki,nchi wanakopitia idadi kubwa ya wakimbizi wanaokimbia vita na mateso."Umoja wa ulaya unabidi uisadie Uturuki kuwahudumia wakimbizi na kufikia ulinzi madhubuti wa mipaka yake ya baharini pamoja na Ugiriki."Amesisitiza kansela Merkel.

Sera kali za kuomba hifadhi ya ukimbizi zaidhinishwa bungeni

Kansela Merkel amewahutubia wabunge hii leo kwa lengo la kuwahimiza wazidishe makali ya sheria za kuomba hifadhi ya ukimbizi.Wabunge 475 wameiunga mkono sheria hiyo iliyowasilishwa na vyama vinavyounda serikali kuu ya muungano mjini Berlin.Sheria hiyo inaruhusu warejeshwe nyumbani haraka wale wote ambao maombi yao ya ukimbizi yatabainika hayana nafasi ya kukubaliwa.

Deutschland Flüchtlinge LaGeSo Berlin
Wakimbizi katika uwanja wa idara ya afya na masuala ya jamii-LaGeSo mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Suala hili hili la waakimbizi ni mojawapo ya mada zinazojadiliwa magharibi hii na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Mbali na suala hilo viongozi watazungumzia pia hali nchini Uturuki na Syria.Wadadisi wanahisi viongozi wa umoja wa ulaya huenda wakawarahisihia waturuki njia za kupata njia ya kuingia katika nchi za umoja wa ulaya.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/epd

Mhariri;Yusuf Saumu