Waasi wayateka makazi ya Gaddafi mjini Tripoli | NRS-Import | DW | 24.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Waasi wayateka makazi ya Gaddafi mjini Tripoli

Madarzeni ya makombora aina ya Grad yamevurumishwa mjini Tripoli mapema leo. Waasi wameyateka makazi ya kanali Gaddafi.

default

Walibya wakishangilia kutekwa kwa makazi ya Gadhafi, Tripoli

Mtu mmoja aliyeshuhudia ameiambia televisheni ya al-Arabiya kwamba barabara ya Al-Sour, karibu na makaazi ya Bab al-Aziziya ya kiongozi wa Libya kanali Muammar Gaddafi, inashambuliwa kwa makombora.

Waasi wameyateka makazi ya Gaddafi na kupandisha bendera yao, lakini hawamkumpata kiongozi huyo wala wanawe. Kumekuwa na shangwe na nderemo katika kiwanja cha Kijani na barabara za mji mkuu Tripoli. Wafuasi wa Gaddafi wangali wanaendeleza upinzani katika baadhi ya sehemu za mji huo, na wanaidhibiti hoteli ya Rixos, makao makuu ya waandishi wa habari wa nchi za kigeni, na wanawazuia wasitoke.

Gaddafi aapa kuichoma Libya

Kufikia sasa Gaddafi hajulikani aliko, lakini amesema katika hotuba iliyotangazwa na redio moja ya Tripoli, na kuripotiwa na televisheni ya Al-Orouba, kwamba kuondoka kwake kutoka makazi yake ni mbinu ya kivita. Gaddafi pia ameapa kufa kama shahidi au apate ushindi dhidi ya jumuiya ya kujihami ya NATO.

Bürgerkrieg in Libyen Erfolg der Rebellen ARCHIV

Kanali Muammar Gaddafi

Msemaji wa Gaddafi, Moussa Ibrahim, amesema kiongozi huyo yuko tayari kupambana na waasi kwa miezi au hata kwa miaka kadhaa na ameapa kuigeuza Libya kuwa volkano na moto. Vikosi vinavyomtii kanali Gaddafi vimevurumisha makombora aina ya Scud katika mji wa Misrata, kutokea ngome yao katika mji wa bandari wa Sirte.

Waasi walikiteka kitongoji cha Abu Salim mjini Tripoli jana jioni, ambacho ni ngome ya wafuasi wa Gaddafi. Msemaji wa waasi hao, kanali Ahmed Bani, ameiambia televisheni ya al Arabiya kuwa wanaamini Gaddafi amejificha katika mojawapo ya maficho yake mengi mjini Tripoli.

Mapigano makali pia yaliendelea kati ya waasi na wafuasi wa Gaddafi kutaka kuudhibiti mji wa Sabha, mji muhimu katika jangwa la kusini mwa Libya, ambao huenda ni ngome ya mwisho ya kiongozi huyo. Kanali Bani ameiambia televisheni ya al Arabiya kwamba waasi wanafanya mazungumzo na viongozi wa kimbari katika mji wa bandari wa Sirte, alikozaliwa Gaddafi, ili waukabidhi mji huo bila umwagaji damu. Waasi wameuteka mji wa Ras Lanuf ulioko katika njia ya kuelekea Sirte.

Libya haitahitaji msaada mkubwa

Mjini Brussels, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema Libya huenda isihitaji msaada mkubwa wa kibinadamu baada ya vita kumalizika kwa kuwa ni nchi tajiri na itapata fedha ambazo zimekuwa zikizuiwa.

"Hii ni kuhakikisha watu wanalipwa, wafanyakazi wa umma, maafisa wa polisi na wengine nakuhakikisha kuna vykula madukani, na kusaidia uchumi kuendelea."

EU Außenministerin Catherine Ashton EU zu Libyen

Catherine Ashton

Fedha zilizowekwa na utawala wa Gaddafi katika nchi za kigeni, zilizuiliwa na Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine ya magharibi, kufuatia hatua ya kiongozi huyo kukandamiza upinzani dhidi ya utawala wake. Bi Ashton amesema Libya ina uwezo wa kuimarisha uchumi wake kwa haraka na hatarajii kutolewa msaada wa kiuchumi kwa ajili ya nchi hiyo.

Ashton amesema wanataka uhuru na demokrasia katika maisha ya kila siku ya Walibya. Amependekeza mkutano mwingine Ijumaa wiki hii mjini New York wa kundi la Cairo kwa ajili ya Libya, mkutano unaowaleta pamoja viongozi wa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na jumuiya ya nchi za Kiarabu. Umoja wa Ulaya utakuwa na jukumu muhimu katika kibarua kigumu cha kukusanya silaha zilizotapaa mjini Tripoli.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, amesema jumuiya ya kujihami ya NATO itaendelea na harakati yake ya kijeshi nchini Libya mpaka usalama utakapoimarika kikamilifu.

Türkei Außenminister Ahmet Davutoglu Tiflis Georgien

Waziri wa kigeni wa Uturuki, Ahmet Davutoglu

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari huko Benghazi, akiwa ameandamana na mwenyekiti wa baraza la kitaifa la mpito, Abdel Jalil, waziri Davutoglu alisema mali za Libya zinazozuiliwa zinapaswa kuachiwa kabla kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani kwa manufaa ya Walibya.

Aliongeza kusema kuwa Walibya wanahitaji fedha kwa dharura kwa ajili ya kuijenga Libya huru na yenye demokrasia. Davutoglu alisisitiza umuhimu wa kuulinda umoja wa Libya na mipaka yake, na kuiahidi Libya msaada kamili wa umma wa Uturuki.

Wafadhili wakutana Doha

Mawaziri wa kigeni wa nchi za kiarabu wamewataka Walibya wajiepushe na kulipiza kisasi kwa ajili ya kuijenga Libya mpya. Mawaziri kutoka Qatar, Saudi Arabia na Misri waliokutana mjini Doha kwenye kikao cha kamati ya amani cha jumuiya ya nchi za kiarabu, pia wamelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa haraka kuachia dola bilioni 2.5 mali za Libya zinazozuiliwa, kulipa mishahara na kugharamia misaada ya kiutu nchini Libya.

Mawaziri hao wamependekeza kulialika baraza la kitaifa la waasi kwenye mkutano wa mawaziri wa kigeni wa jumuiya ya nchi za kiarabu utakaofanyika Jumamosi ijayo, kujadili matukio katika ulimwengu wa kiarabu, ikiwemo Libya na Syria.

Qatar leo itandaa mkutano wa mataifa fadhili kuliwezesha baraza la kitaifa la mpito kupata dola bilioni 2.4 ili kuliwezesha kulipa mishahara ya Walibya kabla siku kuu ya Eid na kugharamia matibabu na miguu bandia inayohitajika na watu waliojeruhiwa.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE/DPAE

Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com