Libya: Tripoli umegubikwa na mapigano | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Libya: Tripoli umegubikwa na mapigano

Umoja wa Kujihami wa NATO umetangaza leo kwamba mwisho wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, uko karibu.

default

Wapiganaji waasi wanalenga shambulio kuelekea uwanja wa Bab al-Aziziya, makao ya Muammar Gaddafi, mjini Tripoli

Umoja wa Kujihami wa NATO umetangaza leo kwamba mwisho wa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, uko karibu, licha ya ukakamavu ulioonyeshwa hadharani na mtoto wa kiume wa kiongozi huyo, Seif al-Islam, ambaye mwanzoni aliripotiwa kuwa amekamatwa. Lakini msemaji wa umoja huo alisema mapigano kati ya waasi na majeshi yanayoiunga mkono serikali yalitwama katika eneo linalozunguka nyumba ya Gaddafi katika mji mkuu wa Tripoli.

Msemaji wa  NATO, Oana Lungescu, aliuwambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Brussles kwamba kwa utawala wa Gaddafi, sasa ni ukurasa wa mwisho, kwani unapigana vita ambavyo umeshindwa. Pia msemaji wa operesheni za kijeshi za NATO kutokea Italy, Kanali Roland Lavoie, alisema  Muammar Gaddafi sio lengo la mashambulio ya NATO, kwani wao haiwalengi watu binafsi. Mapigano makali yaliendelea leo karibu na hoteli ilio na waandishi wa habari wa kigeni mjini Tripoli. Sauti za mizinga mikubwa zimekuwa zikisikika tangu asubuhi karibu na Hoteli ya Rixos. Ni kutoka hoteli hiyo ndiko mwana wa kiume wa Gaddafi, Seif al-Islam, alipotangaza kwamba Muammar Gaddafi na familia yake bado wako Tripoli.

Libyen Gaddafi Sohn Saif al-Islam in Tripolis

Seif al-Islam( katikati), mwana wa kiume wa Muammar Gaddafi, anawapungia watu leo katikati ya mji wa Tripoli, licha ya kuripotiwa kabla kwamba alikamatwa

" Kwanza ni upotovu wote wa maneno. NATO na nchi za Magharibi wanayo teknolojia kubwa na njia za mawasiliano, wametumia risala kwa Walibya kupitia vyombo vya habari vya Libya na kuendesha vita vya elektronik ili kuleta michafuko ya kuidhoofisha Libya."

Kanali Lavoie alikiri kwamba kutekeleza pigo la mwisho dhidi ya majeshi ya Gaddafi mjini Tripoli kunaonekana kuwa ni kugumu zaidi kutokana na majukumu ya NATO, na namna yalivyo mapigano ya mabarabarani katika mji huo. Aliongeza kusema kwamba ni shida kutoa msaada wa kutoka angani moja kwa moja wakati wa mapigano ya mijini yanajiri. Msemaji huyo wa operesheni za NATO alisema wao hawajuwi wapi alipo kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ila kila mtu anatambuwa kwamba Gaddafi huenda sana asiwe sehemu ya suluhisho la mzozo wa Libya, kwani yeye sasa si mchangiaji mkubwa wa suluhisho. Alisema ikiwa Gaddafi ataondoka Libya, hilo halitakuwa ni tatizo kwa  NATO, kwani  jukumu la NATO ni kuwalinda raia wa Libya.

Na kwa mujibu wa mwandishi wa Televisheni ya al-Jazeerah ni kwamba wapiganaji waasi wa Libya wameyazunguka majengo  ya Bab al-Aziziyah ambayo ndio ngome ya Gaddafi, na baadhi ya waasi wameingia kupitia moja ya milango yake. Na katika upande wa mashariki ya Libya, waasi wameuteka mji wa Ras Lanuf na kuwasuka nyuma wapiganaji walio watiifu kwa serikali hadi katika viunga vya mji wa Bin Jawad. Mwandishi wa al-Jazeerah alisema majeshi ya Gaddafi yalikuwa yanarejea nyuma kuelekea mji wa Sirte, alikozaliwa Gaddafi.

Na kwa upande mwengine, vituo viwili vya mpaka wa Libya na Tunisia vimefungwa, lakini kuuvuka mpaka huo kunawezekana kwa msingi  wa kila ombi la mtu kuamuliwa kutokana na uzito wake. Katika saa 24 zilizopita, Walibya waliojeruhiwa wameruhusiwa kuingia Tunisia na kupelekwa hospitali. Na kutoka upande wa Tunisia, familia zilizoshikilia kurejea nyumbani ziliruhusiwa kuuvuka mpaka.

Pia imetangazwa kwamba Malta na Bahrein zimelitambua baraza la mpito la taifa huko Libya kama mwakilishi halali wa wananchi wa Libya.

Mwandishi: Miraji Othman

Mhariri:  Mohammed Abdulrahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com