Waasi Kusini mwa Sudan wakubali kusitisha mapigano | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waasi Kusini mwa Sudan wakubali kusitisha mapigano

Jeshi la Sudan ya kusini limefikia makubaliano muhimu na kundi moja la waasi kusitisha mapigano siku chache kabla ya kura ya maoni

default

Rais wa jamhuri ya Sudan Omar al-Bashir, (kati), akisindikizwa na makamu wake, Salva Kiir Mayardit, alipotembelea mji wa Juba hivi karibuni.

Jeshi la Sudan ya kusini limetia saini makubaliano ya kusitisha mapigano na wapiganaji wa kundi moja lililojitenga jana na kupunguza hali ya wasiwasi wa uwezekano wa kuzuka ghasia siku chache kabla ya eneo hilo kupiga kura muhimu ya maoni kuhusiana na eneo hilo kujitenga ama la.

George Athor, afisa mwandamizi wa zamani katika jeshi la kusini mwa Sudan, amekuwa kiongozi wa mwisho wa kundi la wapiganaji wa chini kwa chini ambaye amekuwa akipigana dhidi ya uongozi wa kusini mwa Sudan. Athor, ambaye anaaminika kuwa amejificha katika maeneo ya msituni ya jimbo la Jonglei, alituma ujumbe ambao ulitia saini makubaliano hayo jana Jumatano katika hoteli moja katika mji mkuu wa eneo la kusini wa Juba.

Majeshi yake yamewauwa wanajeshi kadha wa jeshi la kusini mwa Sudan tangu pale alipojitenga na serikali ya eneo hilo, baada ya kuwashutumu maafisa kwa kufanya udanganyifu katika uchaguzi wa mwezi Aprili.

Tunamshukuru George Athor kwa juhudi zake bila ukomo kufanikisha makubaliano haya ya kusitisha mapigano, amesema afisa wa jeshi Michael Majur, akizungumza kwa niaba ya jeshi la Sudan ya kusini la SPLA.

Upigaji kura ya maoni utaanza Januari 9, ambapo wapigaji kura wanaulizwa iwapo eneo la kusini liwe huru ama la, ikiwa ni kilele cha hatua za kuleta amani ambazo zilianza mwaka 2005 na kumaliza vita virefu kabisa vya wenyewe kwa wenyewe katika bara la Afrika.

Eneo hilo lenye mafuta , lakini ambalo ni masikini la kusini limekuwa halina usalama kutokana na ghasia za kikabila, wanajeshi wasio na nidhamu pamoja na wapiganaji wengine wanaoipinga serikali na kusababisha hali ya wasi wasi kwamba eneo hilo litapata taabu kujitawala.

Kiasi cha wapigakura milioni 3.9 ambao wamejiandikisha , watapiga kura kuanzia Jumapili ijayo, na kuhitimisha miezi kadha ya matayarisho kwa ajili ya kura hiyo ambayo umoja wa mataifa umesema jana kuwa unatarajia utafanyika bila ya matukio mabaya.

Wasudan ya kusini wengine 60,000 wanaoishi nje ya nchi hiyo wamejiandikisha kupiga kura katika nchi nane duniani, ikiwa ni pamoja na Canada, Ethiopia, Marekani , Australia na Uingereza. Waziri wa utamaduni wa kusini mwa Sudan Gabriel Chang alikuwa mmoja wa maafisa wa kusini mwa Sudan jana katika maandamano ya kuwataka watu wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

"Hatua hizi kuelekea uhuru zilianza miaka mingi iliyopita, unaweza kusema tangu mkutano wa Juba mwaka 1947. Hivi sasa tunakaribia kufikia hatua hiyo na tuna siku tatu tu na tukio hili ni tukio la mwisho kuwafahamisha watu wa kusini mwa Sudan , kuwataka kujitokeza kwa wingi kupiga kura ya ndio kwa ajili ya kujitenga".

Upigaji kura unatarajiwa kuendelea hadi Januari 15.

Marekani inaamini kuwa kura hiyo ya maoni kuhusu uhuru wa Sudan ya kusini itafanyika bila matatizo na kwa njia ya amani, amesema afisa mmoja mwandamizi wa Marekani jana.

Kugawanyika kwa nchi hiyo kunatarajiwa na wengi lakini upande wa kaskazini umeahidi kukubali matokeo ya kura hiyo na kupunguza wasi wasi wa kuzuka tena mzozo mpya.

Umoja wa mataifa umesema kuwa zaidi ya waangalizi wa kigeni 1,000 na 15,000 kutoka ndani ya Sudan wataangalia kura hiyo katika vituo 2,700 vya kupigia kura katika Sudan ya kusini pamoja na vituo 175 katika eneo la Sudan ya kaskazini. Matokeo yatapatikana baadaye mwezi wa Februari.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE / DPAE/ RTRE

Mhariri : Josephat Charo

 • Tarehe 06.01.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/zuBy
 • Tarehe 06.01.2011
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/zuBy

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com