1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa dunia wailaani Urusi kuhusu Ukraine

22 Februari 2022

Nchi za magharibi zimeshutumu uamuzi wa rais wa Urusi Vladimir Putin kutambua maeneo mawili yaliyojitenga ya Ukraine kuwa jamhuri. Wakuu wa nchi za magharibi wametaka Urusi kuwekewa vikwazo kufuatia uamuzi huo. 

https://p.dw.com/p/47P3t
USA | UN Sicherheitsrat zur Ukraine
Picha: Evan Schneider/United Nations/AP Photo/picture alliance

Wakuu wa Ufaransa, Ujerumani na Marekani wameilaani hatua ya Putin wakisema ni ukiukwaji wa wazi wa makubaliano ya amani ya Minsk. Kupitia taarifa, ofisi ya kansela wa Ujerumani imesema baada ya mazungumzo kati ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Marekani Joe Biden, viongozi hao wamekubaliana kwamba hatua ya Putin haitakosa kujibiwa.

Soma pia: Mawaziri wa mambo ya nje wa EU wakataa kuiwekea vikwazo Urusi

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield aliikosoa kauli ya Putin kwamba wanajeshi wa Urusi watakuwa na jukumu la kulinda amani tu. Kulingana na Thomas-Greenfield huo ni uwongo mtupu kwani wanajua fika dhamira ya Urusi.

Russland Präsident Putin Dekret zu abtrünnigen Regionen in Ost-Ukraine
Putin ametambua uhuru wa Donetsk na LuhanskPicha: Alexey Nikolsky/Kremlin/SPUTNIK/REUTERS

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uamuzi wa Urusi ni ukiukwaji wa mipaka na uhuru wa Ukraine na unakinzana na maadili ya Umoja wa Mataifa.

Rais wa Ufaransa Emmanuel macron ambaye hadi jana asubuhi alikuwa angali anasisitiza njia ya diplomasia kusuluhisha mzozo huo, ameutaka Umoja wa Ulaya kutoa vikwazo maalum dhidi ya Urusi.

Taarifa kutoka ikulu ya Macron imeongeza kwamba rais huyo ametaka kuandaliwe mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vile vile vikwazo kutoka Ulaya dhidi ya Urusi viidhinishwe.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameupinga uamuzi wa Putin akiutaja kuwa ukiukwaji wa wazi wa uhuru wa Ukraine.  Ameongeza kuwa vikwazo kabambe vitatolewa dhidi ya Urusi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg, amesema uamuzi wa Putin unakiuka uhuru wa Ukraine na mipaka yake. Inahujumu juhudi za kusaka suluhisho la mgogoro huo na vile vile unakinzana na mkataba wa amani wa Minsk ambao Urusi ni mwanachama.

Ukraine Konflikt - Anerkennung von Donezk durch Russland
Watu walisherehekea uamuzi wa Urusi mkoani DonetskPicha: Alexei Alexandrov/AP Photo/picture alliance

Kulingana na Stoltenberg, Urusi inaendelea kuzidisha mvutano mashariki mwa Ukraine kwa kutoa ufadhili wa kifedha kwa waliojitenga nchini Ukraine. Aidha, inajaribu njama ya kuivamia Ukraine kwa mara nyingine.

Viongozi wawili wa ngazi ya juu zaidi katika Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Charles Michel, walitoa taarifa zinazofanana kupitia kurasa zao za twitter.

Wote walilaani hatua ya Putin kama ukiukwaji wa wazi wa sheria ya kimataifa na kwamba Umoja wa Ulaya na washirika wake watachukua hatua ya pamoja, na kushirikiana kwa uthabiti kusimama na Ukraine.

Annalena Baerbock, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema Urusi inaenda kinyume na makubaliano ya amani ya Minsk yaliyosainiwa mwaka 2014. Na kwamba kutokana na uamuzi huo, Urusi imevunja ahadi zake kwa ulimwengu.

Soma pia: Urusi yawakosoa viongozi wa Magharibi kutabiri vita na Ukraine

Kauli nyingine za ukosoaji dhidi ya Putin zimetolewa na Romania, Japan na Australia.

Hata hivyo China ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi haikudhihirisha inasimama upande gani. Kwenye kauli yake imezitaka tu pande husika kwenye mzozo huo kujizuia dhidi ya vitendo vinavyoweza kueneza mgogoro  

(AFPE)