1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaikosoa Magharibi kutabiri vita na Ukraine

Mohammed Khelef
20 Februari 2022

Urusi imeyakosowa mataifa ya Magharibi kusambaza taarifa za khofu zikidai nchi hiyo iko tayari kuivamia Ukraine, huku eneo la mashariki mwa Ukraine likishambuliwa kwa maroketi ambayo hakuna upande uliodai kuhusika.

https://p.dw.com/p/47JGL
Belarus | Russland | gemeinsame Militärübung
Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumapili (Februari 20), msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, alinukuliwa na shirika la habari la Interfax akisema kwa mataifa ya Magharibi kuendelea kutabiri kila siku tarehe ambazo Urusi inapanga kuivamia Ukraine ni uchokozi wazi unaoweza kuwa na matokeo mabaya. 

Hata hivyo, Peskov aliongeza kuwa Rais Vladimr Putin hata hana habari na kauli hizo za mataifa ya Magharibi, akisema kuwa Moscow inategemea uwezo wa washirika wake wa Magharibi kujenga hoja.

Mara kadhaa, viongozi wa Magharibi wamekuwa wakionya kwamba Urusi inajitayarisha kuishambulia Ukraine, ambayo imezungukwa pande zake tatu na wanajeshi wapatao 150,000 wa Kirusi, ndege za kivita na vifaa vya kijeshi.

Luteka za kijeshi za Urusi

Belarus | Russland | gemeinsame Militärübung Union Courage
Helikopta ya jeshi la Belarus katika mazoezi ya pamoja na jeshi la Urusi nchini Belarus.Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumamosi (Februari 19), Urusi ilifanya mazoezi ya silaha zake za nyuklia na luteka nyengine za kawaida katika taifa jirani la Belarus, wakati huo huo ikiendelea na mazoezi ya jeshi lake la majini katika Bahari Nyeusi.

Zote, Urusi na Belarus, zlitangaza siku ya Jumapili kwamba mazoezi yao ya kijeshi nchini Belarus yangeliendelea kutokana na hali ya wasiwasi iliyopo nchini Ukraine.

Kuwepo kwa wanajeshi wa Urusi nchini Belarus kunaifanya Moscow kuwa na idadi kubwa ya wanajeshi kwenye mpaka wa kaskazini mwa Ukraine, kama ilionao tayari kwenye mipaka ya mashariki na magharibi.

Mashambulizi mashariki mwa Ukraine

Russland Rostov Region Ankunft Evakuierte Ostukraine
Watu wakihamishwa kutoka eneo la mashariki mwa Ukraine baada ya mashambulizi ya maroketi na mizinga.Picha: Sergey Pivovarov/REUTERS

Kauli hiyo imetolewa katika wakati ambapo kuna taarifa za mamia ya makombora yaliyorushwa katika eneo la mstari wa mbele wa mapigano kati ya wanajeshi wa Ukraine na waasi wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi, mashariki mwa Ukraine.

Maelfu ya watu wamehamishwa kutoka eneo hilo, baada ya wasiwasi kuzuka kwamba mashambulizi hayo yanaweza kuchochea uingiliaji kati wa Urusi.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba, amesema nchi yake haihusiki na mashambulizi hayo, na badala yake ametaka uchunguzi huru wa kimataifa. 

Kuleba alisema umeshafika wakati kwamba mataifa ya Magharibi kutekeleza angalau sehemu ya vikwazo ambavyo imevitayarisha dhidi ya Urusi. 

"Urusi inapaswa kuzuiwa hivi sasa. Tunaona jinsi mambo yanavyozidi kuibuka hivi," alisema mara baada ya taarifa za mashambulizi hayo kusambaa siku ya Jumapili (Februari 20).

Wakati Waziri Kuleba akisema hayo, Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine amemuomba Rais Putin achaguwe mahala popote anapotaka ili wawili hao waweze kuonana na kuutatuwa mzozo uliopo baina ya nchi zao.

"Ukraine itaendelea kufuata njia ya kidiplomasia pekee kwa maslahi ya suluhisho la amani," alisema Zelensky siku ya Jumamosi (Februari 19) katika Kongamano la Usalama la Munich, Ujerumani.

Hakukuwa na jibu  la moja kwa moja kutoka kwa serikali ya Urusi baada ya ombi hilo la Zelensky.

Marekani na mataifa kadha ya Ulaya yamewataka raia wao kuondoka nchini Ukraine, kufuatia miezi kadhaa ya kuituhumu Urusi kuandaa mazingira yanayochochea uvamizi wake dhidi ya taifa hilo. Viongozi hao wametishia vikwazo vikali na vya ghafla endapo Urusi itaivamia Ukraine.