Vikosi vya Iraq vyazidi kusonga mbele Mosul | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 20.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Vikosi vya Iraq vyazidi kusonga mbele Mosul

Vikosi vya Iraq vinavyoungwa mkono na Marekani, vimefanikiwa kuvikomboa vijiji 15 kutoka mikononi mwa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, baada ya kuanzisha mashambulizi makubwa ya kuukomboa mji wa Mosul.

Vikizidi kusogea mbele kutoka maeneo mbalimbali, vikosi hivyo vimeelekea katika uwanja wa ndege wa Mosul, kusini mwa mji huo. Hii ni operesheni mpya kufanywa na jeshi kubwa la Iraq, katika miaka kadhaa. Hata hivyo, vikosi vya Iraq vimekutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wanamgambo wa IS wanaotaka kuendelea kuudhibiti mji wa Mosul.

Kamanda wa juu wa jeshi ametangaza kuwa vikosi hivyo vimevikomboa vijiji vya kusini mwa Mosul, kikiwemo cha Athbah. Vikosi maalum vya operesheni nchini Iraq, jeshi la kawaida na vitengo vya polisi vya shirikisho vinashiriki katika operesheni hiyo sambamba na vikosi vya jeshi vilivyoidhinishwa na serikali, vingi vikiwa na wapiganaji wa Kishia ambao wanaendesha operesheni kwenye viunga vya mji huo.

Kamanda wa muungano wa majeshi yanaoongozwa na Marekani, Luteni Jenerali, Stephen Townsend amesema mapambano kwenye mji wa Mosul ambao uko chini ya udhibiti wa kundi la IS tangu kipindi cha majira ya joto mwaka 2014, yatakuwa magumu kwa jeshi lolote lile duniani. Kamanda Townsend amesema majeshi hayo yamefanya zaidi ya mashambulizi 10,000 ya anga dhidi ya IS nchini Iraq, na imewapatia mafunzo na vifaa zaidi ya wanajeshi 70,000 wa Iraq.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis amesema vikosi vya muungano vinaunga mkono operesheni hiyo na tayari vinashiriki katika mapambano. 

 General James Mattis (Getty Images for DIRECTV/B. Steffy)

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim Mattis

''Operesheni inayoendelea magharibi mwa Mosul, kama mnavyojua imekuwa ikifanyika kwa muda sasa. Vikosi vya Marekani vinaendelea na majukumu yake yale yale ambayo vimekuwa vikifanya kusini mwa Mosul na vikosi vya muungano vinaunga mkono operesheni hii, na tutaendelea na juhudi za kulisambaratisha kundi la IS,'' amesema Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis.

Mattis ambaye amewasili leo mjini Baghdad katika ziara ambayo haikutangazwa amesema Marekani haiko Iraq kwa ajili ya kutafuta mafuta.

Mwezi uliopita, Iraq ilitangaza kuwa eneo la kusini mwa Mosul limekombolewa kabisa kutoka kwa IS, baada ya mapigano makali yaliyodumu kwa miezi mitatu. Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi jana alitangaza kuwa vikosi vya serikali vinaelekea kuwakomboa watu wa Mosul dhidi ya ukandamizaji na ugaidi unaofanywa na wanamgambo wa IS.

Wakati mashambulizi hayo yakiendelea, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mamia kwa maelfu ya raia waliokwama ndani ya nyumba zao mjini Mosul ''wako katika hatari kubwa'', na wamepungukiwa mafuta, hawana chakula na maji na wanakabiliwa na ukosefu wa umeme.

Nayo mashirika ya kutoa misaada yameelezea wasiwasi wake kuhusu watu hao, wengi wakiaminika kuwa watoto. Shirika la kimataifa la kuwahudimia watoto la Save the Children limesema nusu ya idadi ya watu waliokwama Mosul, ni watoto.

Mratibu wa shirika la misaada ya kibinaadamu la Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Lise Grande, amesema wanaandaa maeneo ya dharura kusini mwa Mosul kwa ajili ya kuzipokea familia zitakazokuwa hazina makaazi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP

Mhariri: Gakuba, Daniel

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com