Uturuki yamtaka Haftar aondoke Sirte | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uturuki yamtaka Haftar aondoke Sirte

Uturuki na Urusi Alhamis zilikubaliana kuendelea kushinikiza usitishwaji wa mapigano Libya ingawa Uturuki inasema Khalifa Haftar, haaminiki na anastahili kuondoka maeneo muhimu ndipo kuweze kupatikana makubaliano.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema pande hizo mbili ambazo zinaunga mkono pande hasimu katika mapigano ya Libya, zimekubaliana kufanya kazi kwa pamoja na kuzisisitizia pande hasimu kutafuta mazingira ya amani ya kudumu na kusitishwa kwa mapigano.

Mshauri mkuu wa usalama wa Rais Erdogan Ibrahim Kalin amesema kwa makubaliano yoyote kufanyika, ni sharti vikosi vya Khaftar viondoke katika mji wa Sirte ambao ni lango kuu la visima vya mafuta Libya na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Jufra ulioko katikati mwa nchi hiyo.

Kuna mvutano mkubwa kwa sasa kati ya nchi zinazounga mkono pande tofauti Libya

Kulingana na taarifa hiyo ujumbe wa Uturuki na Urusi utatafakari kubuni kundi moja la kiufanyia kazi kuhusiana na Libya na wamepangiwa kufanya majadiliano zaidi mjini Moscow katika siku za hivi karibuni.

Erdogan empfängt Libyens Ministerpräsident (picture-alliance/dpa/Turkish Presidency)

Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Saraj

Mkutano huu kati ya Urusi na Uturuki unakuja wakati ambapo kuna mvutano mkubwa kati ya nchi zinazounga mkono pande tofauti katika vita hivyo. Ni wiki hii tu ndipo bunge la Misri lilipitisha kutumwa kwa majeshi nje ya nchi hiyo hatua inayotishia kuchochea vita hivyo na kuzileta Misri na Uturuki katika makabiliano ya moja kwa moja. Ibrahim Kalin anazungumzia hali hiyo.

"Misri kufikiria kutuma majeshi Libya haitosaidia smchakato wa kisiasa hasa wakati ambapo sote tunafanya juhudi za kusitishwa kwa mapigano na kujaribu kuusogeza mchakato wa kisiasa upande huo. Nafikiri litakuwa jambo hatari la kijeshi kwa Misri kufanya," alisema Kalin.

Haftar hatotii usitishwaji wa mapigano Libya

Marekani imesema Urusi imetuma ndege za kivita katika uwanja wa ndege wa Jufra ili kuwasaidia mamluki wa Urusi ambao wanapigana pamoja na jeshi la Haftar. Urusi na jeshi la LNA lake Haftar wote wamekanusha haya.

Ägypten Chalifa Haftar und Abdel-Fattah el-Sissi (picture-alliance/AP Photo/Egyptian Presidency Media office)

Khalifa Haftar (kushoto) akiwa na Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi (kulia)

Lakini mshauri huyo mkuu wa Rais Erdogan katika masuala ya usalama haamini iwapo Haftar atatii usistishwaji mapigano akidai kwamba wahusika wengine huko mashariki mwa Libya wanastahili kuwa na jukumu katika kufanikisha jambo hilo.

"Haftar si mshirika wa kutegemewa, hatumchukulii kama mshirika wa kweli, ila kuna bunge lengine Tobruk. Kuna wahusika wengine Benghazi. Majadiliano yanastahili kufanyika baina yao. Hii ni baina ya makundi ya Libya," alisema Kalin.

Lakini Wizara ya mambo ya nje ya Urusi inasema inaunga mkono usitishwaji wa mapigano na mazungumzo ya kisiasa yatakayoleta uongozi wa pamoja.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com