1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Fedeo na utafiti wake kuhusu Nyerere

20 Agosti 2018

Mtafiti Ignas Fedeo kutoka Tanzania, anachunguza simulizi za Wanyakyusa kuhusu Mwalimu Julius Nyerere kutaka kujua kwanini wanaendelea kumuenzi katika simulizi zao.

https://p.dw.com/p/33RDB
Ignas Fedeo Wissenschaftler an der Makerere University in Uganda
Picha: DW/E. Lubega

Fedeo anachunguza simulizi za Wanyakyusa kuhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kujua kwanini wanaendelea kumuenzi. Ikumbukwe kuwa jamii ya Wanyakyusa haina mahusiano yoyote ya jamii anakotoka mzalendo huyo maarufu wa Afrika. Fedeo ni mmoja kati ya wasomi kutoka Tanzania waliopata ufadhili wa Taasisi ya Gerda Henkel Stiftung ya Ujerumani kusomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. 

Ignas Fedeo amekuwa mwenyeji katika chuo kikuu cha Makerere kilichoko nje kidogo ya kitovu cha mji wa Kampala kwa takriban miaka miwli. Makerere ni miongoni mwa taasisi kongwe na maarufu barani Afrika ambako idadi kubwa ya Wazalendo wa Afrika walipata elimu yao ya juu iliyo changia pakubwa katika kuwandaa kwa kulikomboa bara hilo kutoka kwa minyororo ya wakoloni. Hadi sasa ni taasisi inayowavutia wasomi kutoka mataifa mengine kuja kusomea shahada zao za uzamili na uzamifu. Ignas Fedeo sasa amejiunga katika orodha hiyo nefu ya wasomi.

"Chuo cha Makerere kingali na hadhi yake tokea akina Mwalimu Nyerere waliposomea hapa. Wengi wanatamani kusomea hapa. Hivyo name nilichukua fursa hii nilipoipata,” anasema Fedeo.

Uchu wa Fedeo wa kutaka elimu ya juu

Ila kuna suali ambalo mtu yeyote atajiuliza, nalo ni kwanini Ignas Fedeo akaingiwa na uchu wa kupata elimu ya kiwango cha juu ililhali ana maarifa na tajriba tosha kufanya kazi zenye kipato cha juu. "Nahitajika kusoma elimu ya juu kwa ajili ya kazi yangu kama mhadhiri msaidizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo natakiwa kuwa na shahada ya uzamifu. Na pia ni fahari kubwa hasa kwentu sisi watu tuliotoka vijijini kuwa na elimu ya kiwango cha juu, kwani ni kielelezo cha mafanikio makubwa kwa jamii yangu nzima,” anaeleza Fedeo.

Katika ngazi hii ya elimu ya uzamifu, Fedeo anapaswa kutoa sababu tosha za kuwaridhisha wahadhiri na wasimamizi wake kwa nini utafiti anaolenga kufanya ni muhimu kwa jamii, na utachangia vipi hazina ya maarifa ya wasomi wengine kwa jumla katika siku zijazo. Hatua hiyo ndiyo ya kwanza kabla kuruhusiwa kuendelea na utafiti wake. Pamoja na kutoa  hakikisho kwamba yuko tayari kukabiliana na changamoto zozote wakati wa kuendesha shughuli zake za utafiti. Fedeo anasema alipojitokeza na wazo la kufanya utafiti kuhusu jinsi Wanyakyusa wanavyo muenzi Mwalimu Nyerere katika fasihi yao simulizi, aliungwa mkono na wasomi wenzake. Anaongezea kuwa mbali na wanasiasa na wanahistoria, watu wengi hawamjui Nyerere kupitia kwa wananchi wa kawaida licha ya kuwa na simulizi zao kuhusu Nyerere. Mwalimu Nyerere ni mzalendo mwenye anaeenziwa  si tu miongoni mwa Watanzania, lakini pia kote barani Afrika. Kama kiongozi muasisi wa nchi ya Tanganyika na kisha Tanzania kuna mengi ambayo wasomi wanahitaji kujifunza kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa. Mitazamo ya Nyerere inaweza kuwa mfano mzuri kwa viongozi wa sasa wa bara la Afrika. Jambo muhimu na la msingi kwa uongozi wake ni jinsi alivyoweza kuunganisha makabila ya Tanzania, kuacha wasia wa kisiasa ambao hakuna anayethubutu kuukosoa. Wengi wanauchukulia kuwa ndiyo muelekeo uliostahili kufuatwa ili kuleta matunda wanayoyafurahia Watanzania ikiwemo wale wa jamii ya Wanyakyusa  anapotokea mtafiti wetu Fedeo.

Ignas Fedeo Wissenschaftler an der Makerere University in Uganda
Ignas Fedeo akiwa nje ya jengo la Chuo Kikuu cha Makerere, UgandaPicha: DW/E. Lubega

Umuhimu wa utafiti wa Fedeo

Fedeo ana imani kuwa kutokana na utafiti wake, wasomi zaidi watapata hamasa ya kufuatilia kwa undani tasnifu hii ya fasihi simulizi na pia kufahamu kuwa kazi bado ipo kuhusiana na maisha ya mwalimu Julius Nyerere hata kama imepita miongo miwili tangu alipofariki. Kwa mfano bado tunasubiri kupokea kazi ya fasihi iliyo na kichwa cha "Shujaa Nyerere” ikiangazia Nyerere katika mapambano na vita mbalimbali. Kulingana na Fedeo, visasili vinavyomhusu ‘shujaa' Nyerere vinamtazama kuwa yeye ni shujaa wa kisiasa na kijamii. Taswira mbalimbali zimetumiwa kuonyesha kuwa Nyerere ni shujaa katika imani za wananchi wa Tanzania na wengine wengi nje ya Tanzania. Imebainika kuwa si Wanyakyusa tu walio na simulizi juu ya Nyerere. Katika kila jamii kuna hadithi kama hizo iwe ni katika jamii za Wagondo, Wagogo, Wasukuma na Wamakonde. Ndiyo maana Fedeo anaeleza "tafiti zangu zitavutia watu kuchunguza suala hilo hilo katika makabila zaidi ya mia moja aliyoyaunganisha mwalimu Nyerere.”

Fedeo ni mmoja kati ya wasomi kutoka Tanzania waliopata ufadhili wa Lisa Maskell kutokea Taasisi ya Gerda Henkel ya  Ujerumani kusomea shahada ya uzamifu katika chuo kikuu cha Makerere, Uganda. Amekamilisha utafiti wake wa awali na sasa anajiandaa kwenda kuhojiana na Wanyakyusa ili aweze kukusanya taarifa za kutekeleza utafiti wake. Anatoa hakikisho kuwa licha ya shinikizo la jukumu hilo, yuko tayari kujitokeza na kazi ambayo itaridhisha wahadhiri wake na hata jamii kwa jumla, kuhisi fahari mpya kuhusu hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwandishi: Lubega, Emmanuel

Mhariri: Buwayhid, Yusra