Ushoga katika michezo, kuna hofu ya wachezaji kujitokeza hadharani | Michezo | DW | 04.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ushoga katika michezo, kuna hofu ya wachezaji kujitokeza hadharani

Wanamichezo wengi wanashindwa kujitokeza hadharani na kujitambilisha kuwa wao wanahusiana kimapenzi na watu wa jinsia sawa.

Wanamichezo kutoka Mexico. Huo ni wakati wa ufunguzi wa michezo ya watu wanaohusiana kimapenzi na watu wa jinsia sawa , mashindano yanayofanyika mjini Koln.

Wanamichezo kutoka Mexico. Huo ni wakati wa ufunguzi wa michezo ya watu wanaohusiana kimapenzi na watu wa jinsia sawa , mashindano yanayofanyika mjini Koln.

Wanamichezo wengi wanashindwa kujitokeza hadharani na kujitambulisha kuwa wao wanahusiana kimapenzi na watu wa jinsia zao. Wanamichezo hao hujizuwia sana kila mara hasa inapotokea kuwa amepata mafanikio makubwa katika michezo. Kabla ya hapo kunakuwa tu na uvumi.

Kwa Gareth Thomas hali sio rahisi. Kijana huyu mwenye mwili uliojengeka vizuri kimichezo mwenye uzito wa karibu kilo 100 na urefu wa mita 1 na centimeta 91, mwili wake unatoa ishara. Napambana hadi mwisho. Katika mchezo anaoshiriki wa rugby , yeye ni shujaa, na akiwa ameshiriki mara 100 katika timu ya taifa ni mchezaji anayeshika rekodi kuitumikia timu ya taifa ya Wales. Kwa muda wa miaka 15 amekuwa akijulikana kuwa ni mchezaji mkakamavu na mwenye mabavu duniani, na hakuna mtu aliyedhani kuwa anasiri anayeficha. Thomas ameweka wazi hali yake hiyo , akiwa bado ni mchezaji maarufu. Ndoa yake ilivunjika, lakini wenzake katika timu wanasema, kwetu sisi ni sawa tu. Na kwa hiyo Thomas anamtaka kila mchezaji, hatimaye, aseme ukweli juu ya maisha yake, na mzigo mkubwa atakuwa ameutua.

Lakini hadi sasa bado ni wanamichezo wachache waliochukua hatua kama yake. Hofu ni kubwa mno kwa jinsi wezao watakavyowachukulia, wale wanaopinga, pamoja na mashabiki wao. Katika michezo ya kulipwa, suala hili linahusu pia malipo, hususan katika mikataba ya wadhamini. Michael Lohaus , rais mwenza wa michezo ya watu wanaofanya mapenzi na watu wa jinsia sawa mjini Kolon , anafahamu maamuzi ya makampuni makubwa.

Nimekuwa nikisikia kila mara kutoka makampuni yanayotoa udhamini kuwa watu wanaofanya mapenzi na jinsia sawa hawaruhusiwi kutumia huduma zetu. Huo ndio utaratibu uliopo na Kwa mujibu wa hayo hakuna mtu anayehitaji mwanamume anayehusiana kimapenzi na mwanamume mwenzake ama mwanamke anayehusiana kimapenzi na mwanamke mwenzake kufanya matangazo ya biashara kwa kampuni kama hizo.

Na inaonekana wakati wote kuwa ni tatizo kwa mwanamichezo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu wa jinsia yake, ambapo katika eneo lingine la kijamii kama siasa ama utamaduni , mapenzi baina ya watu wa jinsia moja sio tena kitu cha ajabu. Kwa Herbert Potthoff kutoka katika kituo cha historia ya mashoga kuna hali wakati wote ya chuki bila sababu na hofu ya kujitokeza hadharani.

Katika michezo ya kulipwa ama michezo mbali mbali hali bado iko hivyo, kwamba karibu hakuna mtu aliyeweza kujitokeza hadharani. Soka ndio mchezo ambao unaweza kupigiwa mfano zaidi. Hakuna mtu anayeweza kujitokeza. Na hii inahusu hata michezo mingine.

Ugumu pia anauona Ingrid Blom kutoka katika klabu kubwa kabisa ya wanawake wanaofanya mapenzi na wenzao wa jinsia moja ya Janus SC mjini Koln. Anasema kuwa michezo ni chombo muhimu kinacholeta hofu na kujenga hali ya kujificha.

Hii haihusiani na mwelekeo wa matamanio yangu kimapenzi, hii inahusu kile ninachoweza kukifanya. Ni vile jinsi mtu anavyoweza kushirikiana na wenzake katika timu na kufikia mafanikio.

Baadhi ya wanamichezo wameweza kujitokeza. Hususan Judith Arndt, mshindi wa medali ya fedha katika mchezo wa kuendesha baiskeli katika michezo ya Olimpiki mwaka 2004, ama mchezaji wa tennis Gottfried von Cramm, pamoja na wachezaji wengi wa mchezo wa kuteleza katika bafaru. Na pia rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani, DFB, Theo Zwanziger, anapinga sana chuki dhidi ya watu wanaofanya mapenzi na watu wa jinsia sawa katika mchezo wa kandanda.

Mwandishi : Olivia Fritz / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri : Othman Miraji.

 • Tarehe 04.08.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oc7O
 • Tarehe 04.08.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oc7O