1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Urusi: Tuko tayari kuzungumza na Marekani kuhusu Ukraine

9 Novemba 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema yuko tayari kukutana kwa majadiliano na mwenzake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio kuhusu kutafuta suluhisho la vita nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/53L1K
Urusi imesema iko tayari kuzungumza na Marekani kuhusu Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov.Picha: Shamil Zhumatov/REUTERS

Ameyasema hayo katika mahojiano na shirika la Habari la RIA Novosti Jumapili. Hata hivyo Lavrov amesema maslahi ya Urusi yatapaswa kuzingatiwa ili amani irejee Ukraine. 

Ameongeza kuwa yeye na Rubio wanafahamu umuhimu wa kujadili suala hilo na kuzingatia ajenda ya pande mbili ndiyo sababu wanawasiliana kwa njia ya simu na sasa wako tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana.

Pendekezo la Putin kuhusu udhibiti wa silaha za nyuklia limefika Marekani

Wakati huo huo Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Urusi amesema Marekani imeiarifu nchi yake kuwa inalipitia pendekezo la Rais Vladimir Putin la kuzingatia udhibiti wa silaha za nyuklia kama ilivyoainishwa katika mkataba mpya wa kudhibiti silaha hizo.

Licha ya hilo, Lavrov amekiri kuwa bado Urusi haijapokea majibu yoyote kutoka Marekani japokuwa vyanzo vya kidiplomasia vimesema kuwa suala hilo linatathminiwa.