1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Upinzani wakosoa kauli ya msajili wa vyama

George Njogopa7 Septemba 2021

Baada ya msajili wa vyama vya siasa kuvitaka vyama kuacha kufanya makongamano,vyama vya upinzani nchini Tanzania vimeipinga na kuikosoa vikali kauli hiyo.

https://p.dw.com/p/4010u
Tansania Wahlen 2020 | Tundu Lissu
Picha: AFP

Hapo jana, msajili huyo, Jaji Francis Mutungi,  alisema yuko mbioni kuitisha mkutano wa pamoja baina ya pande hizo kwa ajili ya majadiliano na hatimaye kumaliza msuguano unajiotokeza mara kwa mara. Lakini wakati akipanga kikao hicho, Msajili huyo alitaka shughuli zote, kama vile makongamano, zisimamishwe kwanza hadi utakapomalizika mkutano wake huo wa maridhiano.

''Nisinge penda kusikia kesho tena kuna kongamano linaandaliwa mahali. Ebu watupe nafasi '', alisema Mutungi. 

Ingawa baadhi ya wachambuzi wanaona kwamba hatua ya msajili kutaka kuzileta pamoja pande zote kwenye meza ya maridhiano ni ya kuungwa mkono, vyama vya siasa na wakosoaji wengi wanahoji ukimya wa ofisi yake katika kushunghulikia kadhia hiyo wakati vyama hivyo vikikumbana na zuio la kufanya shughuli zao lililowekwa tangu mwanzoni mwa utawala uliopita wa Marehemu Rais John Magufuli na kuendelezwa hadi sasa.

Chadema, ambacho kimejikuta kikilazimika kusitisha vuguvugu lake la kudai mabadiko ya katiba mpya kutokana na kubanwa na vyombo vya dola, ni miongoni mwa vyama vilivyokosoa kauli ya msajili huyo, na kulingana na mkurugenzi wake wa uenezi, mawasiliano na mambo ya nje, John Mrema, jambo hilo halikubaliki.

''Yeye alipaswa kwanza awambie polisi waache kuvizuwiya vyama vya siasa kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kisheria.Na sio kuviambia vyama visubiri'',alisema Mrema.

''Msajili angienda mbali zaidi,tukutane na rais ''

Mazingira ufanyaji siasa kwa vyama vya upinzani imekuwa ni ya mashaka mashaka
Mazingira ufanyaji siasa kwa vyama vya upinzani imekuwa ni ya mashaka mashaka Picha: DW/S. Khamis

Nacho cha cha NCCR-Mageuzi ambacho hivi karibuni kilijikuta kikishindwa kufanya mkutano wake wa ndani wa kamati kuu baada kutokana na kuzingirwa na jeshi la polisi kimeingia katika orodha ya kuishutumu kauli ya Jaji Mutingi. Huyu hapa ni mkuu wa idara ya uenezi na mawasiliano ya umma wa chama hicho, Edward Simbeye.

''Mimi nilidhani msajili angienda mbali zaidi,atuambiye sisi tukutane na waziri mwenye dhamana zaidi, tukutane na rais kwa ajili ya kuzungumza haya mamabo ambayo yanaendelea katika nchi yetu.'',alisema Simbiye.

Kumekuwa na mgawanyiko wa kimaoni tangu msajili wa vyama kuonyesha nia ya kutaka kuzileta pamoja pande hizo na hasa kutokana na msisitizo wake wa kumaliza uhasama baina ya polisi na vyama vya upinzani. Hii ni kutokana na taswira ambayo vyama vya upinzani vinamuangalia msajili huyo na ofisi yake.

Kwa muda mrefu, mazingira ufanyaji siasa kwa vyama vya upinzani imekuwa ni ya mashaka mashaka na mara nyingi  mikusanyiko yao imekuwa ikisambaratishwa na jeshi la polisi.

Endapo hatua ya msajili wa vyama vya siasa kusaka maridhiano baina ya polisi na vyama hivyo itafungua ukurasa mpya, ni jambo la kusubiri na kuona.