1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya,China na Urusi zasimama na Iran

Saumu Mwasimba
25 Septemba 2018

Nchi hizo zimeafikiana kuanzisha taasisi huru ya kisheria itayoratibu shughuli za kibenki katika biashara na Iran baada ya Marekani kujiondowa katika mkataba wa Nuklia wa Iran

https://p.dw.com/p/35Rsr
USA P5+1 Gespräche in New York über den Atom-Abkommen mit dem Iran | Mogherini und Zarif
Picha: picture_alliance/dpa/A. Shcherbak

Ulaya,Urusi na China zimejiweka katika nafasi ya kuvutana na rais wa Marekani Donald Trump baada ya hapo jana usiku kutangaza mipango ya kuunda njia maalum za kurahisisha shughuli za kibiashara na Iran,hatua ambayo inakiuka vikwazo vya Marekani.

Baada ya mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini kukutana na wajumbe kutoka Uingereza,Ufanasa,Ujerumani ,Urusi China na Iran hapo jana alitangaza kwamba nchi hizo ambazo zote zimesaini makubaliano ya Nuklia ya Iran zimefikia uamuzi wa kuendelea na shughuli za kibiashara na Iran.Akafafanua zaidi kwa kusema:

''Washiriki wamesisitiza haja ya kulinda uhuru wa uendeshaji wa kiuchumi ili kuwa na fursa ya kufanya biashara kwa njia halali na Iran kwa kuzingatia kwa ukamilifu azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa nambari 2231''

Maamuzi yaliyofikiwa na nchi hiyo yanamaanisha kwamba sasa Umoja wa Ulaya utaunda taasisi huru ya kisehria ambayo itaratibu shughuli kutowa na kupokea malipo ya fedha katika shughuli za kibiashara na Iran.

Mogherini aliendelea kusema kwamba kundi hilo la nchi Umoja wa Ulaya,China na Urusi  zimeidhinisha kwa kauli moja mapendekezo ya kiutendaji ya kuendelea kuzibakisha na kuziimarisha njia za kurahisisha mchakato wa malipo  yanayohusiana na biashara na Iran ikiwemo biashara ya mafuta.

Nchi zote zilizoshiriki katika mkutano uliofikia maamuzi hayo jana ziliafiki kwamba Iran inatekeleza majukumu yake kama sehemu ya mkataba wa Nyuklia uliosainiwa 2015 na hilo limethibitishwa katika ripoti 12 mfululizo zilizowahi kutolewa na shirika la kimataifa la Atomiki IAEA.

Donald Trump
Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Lakini hatua iliyochukuliwa na nchi hizo ni dhahiri inaweka mazingira ya kuzuka mvutano mkubwa na Marekani ambayo iliiwekea tena vikwazo Iran mnamo mwezi Agosti ambavyo pia vinataja kwamba nchi yoyote au makampuni yatakayoshirikiana kibiashara  na Iran yataadhibiwa. Duru nyingine ya vikwazo vya Marekani kuelekea Iran inatarajiwa kutangazwa mwezi Novemba na hasa vikilenga kukwamisha kabisa usafirishaji wa mafuta wa jamhuri hiyo ya kiislamu.

 Vikwazo hivyo vitamaanisha kwamba makampuni zaidi makubwa yatalazimika kuamua ama kuondowa vitega uchumi vyao Iran au kupoteza fursa zao za kibiashara na Marekani. Jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alifanya mkutano na waandishi habari akasema kwamba rais Trump atatumia nafasi yake kama mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuzitolea mwito nchi zote kuunga mkono kampeini ya kuishinikiza Iran katika mpango wake wa Nyuklia. Uamuzi huo wa Marekani  lakini huenda ukasabababisha cheche za moto na wanachama wengine wa baraza la usalama la Umoja huo wa Mataifa,Uingereza,Ufaransa China na Urusi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman