1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

UN yataka Marekani, Israel na Iran zisitishe mapigano

3 Machi 2026

Umoja wa Mataifa umezitolea wito pande zote zinazohusika kusitisha mapigano katika eneo la Mashariki ya Kati wakati ambapo hofu na taharuki vinaendelea kutanda kwenye ukanda huo.

https://p.dw.com/p/59jo0
Umoja wa Mataifa umetaka vita visitishwe Mashariki ya Kati
Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa Ravina Shamdasani Picha: Fatih Erel/AA/picture alliance

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk kupitia msemaji wake Ravina Shamdasani amesema ameshtushwa na namna mzozo huo unavyoendelea kuwaathiri raia.

Shamdasani amezikumbusha pande hizo kuhusu sheria ya kimataifa inayoweka wazi kuwa raia pamoja na makazi yao hawapaswi kushambuliwa na kuwa sheria hiyo inapaswa kuheshimiwa.

Iran yataka Umoja wa Mataifa uchukue hatua kumaliza vita

Wakati huohuo, Iran imelitolea wito Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua ili kuvimaliza vita kati ya nchi hiyo, Marekani na Israel.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje Esmail Baqaei amesema kuwa, "Umoja wa Mataifa una wajibu, unaweza kuchukua hatua kama ukipenda kwa sababu hakuna kikwazo cha kuchukua hatua isipokuwa tu nia yake ya kufanya hivyo."

Baqei ameyaonya pia mataifa ya Ulaya yasithubutu kujiunga na vita vinavyoendelea vinginevyo hatua za aina hiyo zitachukuliwa kama vita dhidi ya Iran.