1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya wataka uchunguzi Gaza

Mohammed Khelef
1 Aprili 2018

Umoja wa Ulaya umeungana na Umoja wa Mataifa kutaka uchunguzi huru juu ya mauaji dhidi ya Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza katika maandamanoo yanayoendelea ya kudai haki ya Wapalestina kurejea nyumbani.

https://p.dw.com/p/2vJh6
Sitzung UN Sicherheitsrat zu Gaza-Unruhen
Picha: picture-alliance/AP/M. Altaffer

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, ametaka uchunguzi wenye uwazi kuhusu nguvu za ziada zilizotumiwa na jeshi la Israel dhidi ya maandamano yanayoendelea karibu na mpaka kati ya Ukanda wa Gaza na Israel.

Hadi sasa, vikosi vya usalama vya Israel vimeshawauwa Wapalestina wasiopungua 16 na kuwajeruhi wengine 1400, wakiwemo 750 waliopata majeraha ya risasi za moto, kitendo ambacho kimesifiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akisema kilikuwa ni cha kujilinda. 

Waandamanaji wa Kipalestina waliviringisha matairi yanayowaka moto na kuwarushia mawe wanajeshi wa Israel, ambao walijibu kwa risasi na gesi ya kutoa machozi.

Mamlaka ya Wapalestina na Uturuki wameishutumu Israel  kutumia nguvu kupita kiasi. 

Mogherini amesema katika kauli yake, kwamba ingawa Umoja wa Ulaya unatambua haki ya Israel kuwalinda raia wake, lazima muda wote kutumia nguvu za kiasi.

Marekani yazuwia azimio la Baraza la Usalama

Haya yanakuja, baada ya Marekani kuzuia rasimu ya kauli ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iliyotaka kutoa wito wa pande zote kujizuwia na mashambulizi na kuitisha uchunguzi juu ya makabiliano hayo ya Gaza.

Kuwait, ambayo inawakilisha nchi za Kiarabu kwenye Baraza la Usalama, iliwasilisha tamko hilo, ambalo lilitaka pia uchunguzi wa uwazi kuhusu ghasia hizo.

Rasimu ya tamko hilo inaelezea pia "wasiwasi mkubwa kutokana na hali ilivyo mpakani" mwa Ukanda wa Gaza na Israel, huku pia likisema ni hali ya raia kuandamana kwa amani. 

"Baraza la Usalama linasikitishwa na kupotea kwa maisha ya Wapalestina wasiokuwa na hatia," inasema sehemu ya rasimu ya tamko hilo iliyosambazwa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama siku ya Ijumaa (Machi 31), lakini mapema Jumamosi, Marekani ikazua vipingamizi, ikisema haitaliunga mkono.

Rasimu hiyo ilikuwa pia inatoa wito kwa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za haki za binaadamu na kiutu, "ikiwemo ya kuwalinda raia," kwa mujibu wa shirika la habari la AFP ambalo liliiona rasimu yenyewe.

Wapalestina wazika wahanga wao

Wakati Marekani ikizuwia kutolewa kwa tamko hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwenye Ukanda wa Gaza,
Wapalestina wameendelea kuwazika wapendwa wao waliouawa na vikosi vya Israel kwenye maandamano hayo, wakitoa wito wa "kulipiza kisasi".

Kundi la Hamas, ambalo ndilo linalotawala Ukanda wa Gaza, lilisema kuwa watano kati ya watu 16 waliouawa ni wanachama wake waliokuwa wakishiriki "matukio ya umma, bega kwa bega na watu wao."

Katika taarifa yake, jeshi la Israel lilisema kuwa 10 kati ya Wapalestina lililowauwa wana historia ya kigaidi kwenye kundi la Hamas na makundi mengine na "waliuawa wakati wakifanya vitendo vya kigaidi."

Msemaji wa jeshi la Israel, Brigedia Jenerali Ronen Manelis, ametishia kutuma wanajeshi ndani ya ardhi ya Gaza endapo kile anachokiita "ugaidi" kwenye maandamano haya, utaendelea. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba
 

Israel Palästina | Proteste am "Tag der Trauer" | Hebron
Jeshi la Israel linashukiwa kuwauwa waandamanaji 16 wa Kipalestina.Picha: picture alliance/AA/M. Wazwaz
Israel Palästina | Proteste am "Tag der Trauer" | Hebron
Kijana wa Kipalestina akirusha jiwe baada ya kupigwa mabomu ya machozi na jeshi la Israel.Picha: picture alliance/ZUMAPRESS/W. Hashlamoun