1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika walaani mapinduzi ya nchini Burkina Faso.

Zainab Aziz Mhariri: Bakari Ubena
1 Oktoba 2022

Umoja wa Afrika siku ya Jumamosi umelaani mabadiliko ya serikali nchini Burkina Faso. Mapinduzi hayo ni ya pili ndani ya mwaka huu wa 2022 katika nchi hiyo maskini ya Afrika.

https://p.dw.com/p/4Hd8C
Burkina Faso | Militärputsch
Picha: RADIO TELEVISION BURKINA FASO/REUTERS

Maafisa wa ngazi ya chini walimpindua kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba mnamo siku ya Ijumaa, wakidai kwamba ameshindwa kupambana na mashambulizi ya watu wenye itikadi kali nchini humo. Wanajeshi hao walimtangaza Kapteni Ibrahim Traore mwenye umri wa miaka 34 kuwa msimamizi.

Anayezungumza: Kiongozi wa Burkina Faso Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba aliyepinduliwa.
Anayezungumza: Kiongozi wa Burkina Faso Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba aliyepinduliwa.Picha: BURKINA FASO PRESIDENCY/REUTERS

Mnamo mwezi Januari, Damiba alijiweka kama kiongozi wa nchi ya milioni 16 baada ya kumshutumu rais mteule Roch Marc Christian Kabore kwa kushindwa kupambana na makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali. 

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat ametoa wito kwa jeshi kujiepusha na vitendo vyovyote vya unyanyasaji, vitisho kwa raia, kubinya uhuru wa rai ana uvunjaji wa haki za binadamu. Katika taarifa yake, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ameagiza kurejeshwa mara moja utaratibu wa kikatiba nchini Burkina Faso.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat Picha: John Thys/AFP

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Moussa Faki Mahamat ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuibuka upya mapinduzi yaliyo kinyume na katiba katika taifa hilo la Afrika Magharibi na kwingineko barani Afrika.

Katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou, hali ya utulivu ilikuwepo kwa muda mfupi tu huku wanajeshi walio kwenye magari ya kivita na yale ya aina ya Pickup wakiendelea kuweka ulinzi kwenye kituo cha televisheni cha taifa na katika maeneo mengine usafiri umeanza kurejea taratibu kwenye barabara za jiji. Hata hivyo kuna taarifa kuwa milio ya risasi imeanza kusika tena katika jiji hilo na hivyo kusababisha wasiwasi.

Wanajeshi wakiweka doria katija jiji la Ouagadougou
Wanajeshi wakiweka doria katija jiji la OuagadougouPicha: Olympia De Maismont/AFP

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imekemea mapinduzi hayo kwa maneno makali na kuyaita kuwa ni unyakuzi wa mamlaka, usiofaa wakati ambapo hatua zilikuwa zimepigwa kwa ajili ya kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba ifikapo Julai 1, 2024.

Ufaransa, mtawala wa zamani wa kikoloni wa Burkina Faso imewataka raia wake wapatao kati ya 4000 na 5000 walio katika mji wa Ouagadougou wabakie majumbani. Umoja wa Ulaya umesema una wasiwasi na matukio hao.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amesema mapinduzi hayo yanahatarisha juhudi za kusimamia mabadiliko, zilizofanywa kwa miezi kadhaa, na kundi la kikanda la ECOWAS. Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa mamlaka kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa Julai 3 ili Burkina Faso iweze kurejesha utaratibu wa kikatiba.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell Picha: European Union

Marekani imetoa wito wa kurejeshwa kwa utulivu haraka na imewataka wahusika wote kujizuia na matendo ya kuvuruga usalama.

Wakati ambapo sehemu kubwa ya eneo la Sahel inapambana na ongezeko la waasi wa makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali, ghasia hizo zimesababisha mfululizo wa mapinduzi kataika nchi za Mali, Guinea na Chad tangu mwaka 2020.

Chanzo:AFP