Umasikini wazidi Marekani | Magazetini | DW | 15.09.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Umasikini wazidi Marekani

Kwa uchache wahariri wamejishugulisha na masuala matatu makubwa, yakiwemo ya kuongezeka kwa umasikini nchini Marekani na ushiriki wa China katika mzozo wa madeni kwenye eneo la sarafu ya Euro.

Wasio na ajira waongezela nchini Marekani

Wasio na ajira waongezela nchini Marekani

Mhariri wa gazeti la Neue Westfälische anasema kwamba hisabu kutoka soko la ajira la Marekani na takwimu ya umasikini zinapandisha kiwango cha wasiwasi. Mmoja katika kila Wamarekani sita aidha ana kazi isiyokimu maisha yake au hata hiyo hana kabisa. Maana yake ni kuwa wengi wanaishi chini ya mstari wa umasikini.

Hakuna suala la mjadala hapa: kwamba unapokuwa una watu wengi wasiokuwa na kazi, maana yake una umasikini uliotitia. Na kwa Wamarekani, waliozowea maisha yasiyo na mikiki, ya kufikiria mlo mmoja kwa siku, huku ni kudhalilika mno.

Itakumbukwa kwamba Marekani bado inajaribu kujijenga tena upya baada ya mtikisiko mkubwa wa kiuchumi wa miaka mitatu iliyopita, ambao uliijeruhi vibaya.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na naibu wake, Phillip Rösler

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) na naibu wake, Phillip Rösler

Naye mhariri wa gazeti la Oldenburgische Volkszeitung anazungumzia sura nyengine ya mgogoro wa kiuchumi na kifedha, tena hapa Ujerumani, unavyogeuka kuwa mgogoro wa kisiasa. Muungano wa vyama vya CDU/CSU na FDP unaounda serikali ya mseto uko hatarini.

Muungano huo unadidimia chini siku hadi siku kiasi ya kwamba majira haya ya mapukutiko ya mwaka 2011, yanakhofiwa kwamba hayatamalizika salama.

Na kiini hasa ni muono tofauti linapokuja suala la Ugiriki. Je, Ujerumani iendelee kubeba mzigo au iutuwe? Je, iendelee kujifanya rafiki wakati wa dhiki ya Wagiriki au iitake Ugiriki isimame kwa miguu yake yenyewe?

Kansela Angela Merkel, anayetoka vyama vya vya CDU/CSU anaamini bado uwezekano wa kuifufua Ugiriki upo, lakini naibu wake, Phillip Rösler kutoka Chama cha FDP anaonekana kuishiwa na stahmala.

Lakini wakati viongozi wa serikali ya mseto ya Ujerumani wakitofautiana juu ya kiasi gani Ujerumani itaendelea kujiingiza kwenye mgogoro wa madeni katika eneo la sarafu ya Euro, wenzao wa China wanajua nini cha kufanya.

Kwa mujibu wa mhariri wa Rhein-Neckar-Zeitung, isingelikuwa China, basi Marekani ingelikwishafilisika kitambo mno. Ndio maana sasa dola hiyo inayoinukia kuwa tajiri mkubwa ulimwenguni inataka kuzinunua dhamana za madeni ya Ulaya. Tayari Italia imeshanyoosha kibakuli cha kuomba msaada kwa Wachina.

Huko nyuma, tayari Ureno, Ugiriki na Hungary zilishaonesha muelekeo huo huo. Na China imeshasema kwamba iko tayari hata kuinusuru nchi nyengine yoyote ya eneo la sarafu ya Euro, zikiwemo Hispania na Ireland.

Lakini kama ilivyo kawaida, anasema mhariri wa Rhein-Neckar-Zeitung, na huu wa China nao una maslahi yake ya kisiasa na kiuchumi.

Vyanzo: Neue Westfälische/Oldenburgische Volkszeitung/Rhein-Neckar-Zeitung
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com