Ujerumani yatangaza mikakati mipya ya usalama | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yatangaza mikakati mipya ya usalama

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere ametangaza mipango ya kuboresha usalama, ikiwemo mamlaka zaidi kwa serikali kuu katika masuala ya polisi upelelezi wa ndani na uhamiaji.

Deutschland PK Terrorverdächtiger Anis Amri in Mailand erschossen Thomas de Maiziere (Getty Images/AFP/T. Schwarz)

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere

Hofu juu ya hali ya usalama imekuwa ikiongezeka miongoni mwa wajerumani kufuatia shambulizi la tarehe 19 Desemba mjini Berlin, na hilo linadhihirika wazi katika utafiti wa maoni na kushamiri kwa mijadala baada ya shambulizi hilo. 

Mwanzo wa mwaka huu wa 2017 unashuhudia malumbano baina ya vyama vya kisiasa, kila kimoja kikijaribu kuja na mapendekezo mapya.

Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere amekuja na mkakati, ambao msingi wake ni kuiongezea serikali ya shirikisho mamlaka katika masuala ya usalama.

Mkakati huo unalenga kuiongezea nguvu polisi ya shirikisho, na kuyaweka majukumu ya huduma za upelelezi mikononi mwa serikali kuu mjini Berlin. Hadi sasa majukumu hayo yalikuwa yakishughulikiwa na mamlaka za majimbo 16 yanayoiunda nchi hiyo.

Jukumu jingine ambalo limekuwa mikononi mwa serikali za majimbo ambalo waziri de Maiziere anataka lihamishiwe serikali kuu, ni la kuwafukuza kutoka Ujerumani watu wanaotafuta hifadhi ambao maombi yao yanakataliwa. Ikiwa hilo litafanikiwa, vituo vya watu waliokataliwa hifadhi vitawekwa karibu na viwanja vya ndege, kuharakisha kuondolewa kwao.

Vyama vingine vyaja juu

Deutschland Sicherheitsmaßnahmen Weihnachtmarkt am Breitscheidplatz (Reuters/H. Hanschke)

Usalama umeimarishwa Ujerumani kufuatia shambulio la mjini Berlin

Hapo jana chama cha Social Democrats SPD ambacho ni mshirika katika serikali ya Kansela Angela Merkel kilitoa mapendekezo yake kuhusu namna ya kuboresha usalama wa ndani. Mapendekezo hayo yanajikita juu ya kuzuia mashambulizi kabla hayajatokea, na kuishirikisha jamii ya waislamu. Chama hicho kinasema hakiamini kuwa matumizi ya polisi tu na kuharakisha kuwafukuza waliokataliwa hifadhi, vinatosha kupambana na ugaidi.

Mwenyekiti wa chama hicho Sigmar Gabriel ambaye pia ni naibu kansela, amepinga vikali mapendekezo ya waziri de Maiziere.

''Mapendekezo ya bwana de Maiziere si chochote zaidi ya kuunda tume pana ya shirikisho, ambamo mamlaka ya majimbo na za shirikisho zitakaa na kubadilishana mawazo kuhusu taasisi za serikali. Siamini kwamba hiyo ni njia muafaka ya kukabiliana na kitisho cha sasa cha ugaidi.'' Amesema Gabriel.

Hata Andreas Scheuer katibu mkuu wa chama cha Christian Social Union, CSU ambacho ni ndugu wa chama cha CDU anachotoka de Maiziere, ameyapinga mapendekezo ya waziri huo, akisema kuyahamishahamisha mamlaka kutoka majimboni hadi serikali kuu itakuwa hatua isiyosaidia kitu.

Kwenda kinyume na katiba

Chama cha mrengo wa kushoto, die Linke kupitia mtaalamu wake wa masuala ya ndani Ulla Jelpke, kimesema mapendekezo ya waziri de Maiziere hayawezekani kikatiba.

''Kulingana na mapendekezo hayo, kila kitu kitakuwa kikishughulikiwa na serikali kuu, kufuata sera za aliyeko madarakani. Nadhani kikatiba ni vigumu kuliamini hilo. Ni kashfa kuona kwamba mamlaka ya serikali za majimbo yakishambuliwa''. Amesema mtaalamu huyo.

Mapendekezo hayo ya waziri wa mambo ya ndani, yanatarajiwa kuchangia katika mdahalo kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Ujerumani baadaye mwaka huu.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dw

Mhariri: Bruce Amani

http://www.dw.com/en/domestic-security-thomas-de-maizieres-2017-wish-list/a-36993577

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com