1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaonya dhidi ya kususia nishati ya Urusi

Lilian Mtono
23 Machi 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza kupinga vikali hatua ya kususia bidhaa za nishati kutoka Urusi na kusema hatua zaidi zitaibua hatari ya matokeo mabaya katika uchumi wa Ulaya. 

https://p.dw.com/p/48v09
Deutschland | Olaf Scholz bei der Generaldebatte im Bundestag
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela Olaf Scholz amesema vikwazo ambavyo tayari vimewekwa dhidi ya taifa hilo vina athari kubwa. Scholz amesisitiza hayo katika wakati ambapo kuna mashaka kwamba hatua zaidi zitaibua hatari ya matokeo mabaya katika uchumi wa Ulaya.

Kansela Scholz amesema hayo wakati kukiwa na miito kwa mataifa ya magharibi kususia kabisa bidhaa zote za nishati kutoka Urusi baada ya kuivamia Ukraine. Scholz amesema ni lazima wawe wazi katika hilo kwa kuwa linaweza kuibua mzozo wa muda mrefu, na mataifa hayo yote yanapaswa kuungana.

Msimamo wa Ujerumani katika hili haubadiliki. Kwa bahati mbaya hili lina ukweli kwa wanachama wengine wengi tu wanaotegemea zaidi makaa, gesi na mafuta, kuliko hata Ujerumani. Na katika hili, hakuna yoyote atakayeachwa nje, alisema Scholz. 

Marekani na washirika wake wa magharibi wanaangazia iwapo Urusi inaweza kusalia katika kundi la mataifa yenye nguvu kiuchumi la G20, baada ya uvamizi huo hii ikiwa ni kulingana na chanzo kilichohusika kwenye majadiliano kuhusu hatua hiyo, kilichozungumza na shirika la habari la Reuters siku ya jana.

Indonesien Jakarta G20 Finanzminister Treffen
Mkutano wa G20 unatarajiwa kufanyika nchini Indonesia, lakini kukiwa na wasiwasi wa baadhi ya wanachama kutoshirikiPicha: Mast Irham/epa/AP/picture alliance

Chanzo hicho kimesema kufuatia uwezekano kwamba jaribio la kuitenga Urusi mara moja huenda likapigiwa kura ya turufu na wajumbe wengine wa kundi hilo ambao ni pamoja na China, India, Saudi Arabia na wengine, kuna mashaka kwa upande mwingine kwamba baadhi ya mataifa pia hayatahudhuria baadhi ya mikutano ya G20 kwa mwaka huu.  

Kundi hilo la G20 pamoja na kundi dogo la mataifa saba ambayo ni Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada, Japan na Uingereza ndio hasa waratibu wa kimataifa katika kila jambo kuanzia hatua kuelekea mabadiliko ya tabianchi hadi deni la kimataifa. 

Wakati mataifa hayo ya magharibi yakifikiria kuiengua Urusi kutoka G20, balozi wa Urusi nchini Indonesia amesema mapema leo kwamba, rais Vladimir Putin anapanga kuhudhuria mkutano wa kilele wa kundi hilo utakaofanyika Indonesia baadae mwaka huu.

USA Präsident Joe Biden
rais Joe Biden wa Marekani atazuru Ulaya kwa nia ya kuimarisha mahusiano na washirika wake wa magharibiPicha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Rais Joe Biden, kuzuru Ulaya kuimarisha uhusiano.

Rais Joe Biden wa Marekani kwa upande wake anaondoka hii leo kuelekea Ulaya akiwa na malengo ya kuimarisha mahusiano na washirika wake wa magharibi, kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi lakini pia likiwa ni jaribio la kuhujumu mzani wa nguvu za kijeshi wa baada ya enzi za vita baridi.

Kesho Alhamisi, Biden  atahudhuria mikutano ya kilele ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO na ule wa mataifa yaliyostawi zaidi kiuchumi ulimwenguni, G7. Biden pia atahudhuria mkutano wa Baraza la Ulaya. Siku ya Ijumaa, atakwenda Poland inayopakana na Ukraine, siku ya Jumamosi akitarajiwa kukutana na rais Andrej Duda.

Huku hayo yakitarajiwa, Umoja wa Mataifa hii leo linajadili maazimio matatu kuhusiana na kuzorota kwa hali ya kibinaadamu nchini Ukraine baada ya Urusi kuamua kuitisha kura kuhusu azimio lake kwenya baraza la usalama, ambalo halitaji mashambulizi yake dhidi ya jirani yake Ukraine. Baraza kuu la Umoja huo limeanza kuangazia maazimio ya wapinzani hao wawili mapema leo, moja linaloungwa mkono na Ukraine na mataifa ya magharibi kwamba Urusi inahusika na kusambaa kwa mzozo wa kibinaadamu na lingine lililodhaminiwa na Afrika Kusini, ambalo haliitaji Urusi.

Soma Zaidi: Guterres aitolea mwito Urusi kumaliza vita Ukraine