1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaahidi misaada zaidi kwa Uturuki na Syria

22 Februari 2023

Ujerumani imeahidi kuongeza maradufu msaada wake nchini Uturuki na Syria kwa kutoa euro milioni 50 zaidi kuwasaidia wahanga wa tetemeko baya la ardhi lililotokea wiki mbili zilizopita na kusababisha maafa makubwa.

https://p.dw.com/p/4NoVY
Türkei Außenministerin Annalena Baerbock und und Innenministerin Nancy Faeser in der Türkei
Picha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Msaada huo wa kifedha umetangazwa na mawaziri wawili, Annalena Baerbock ambaye ni waziri wa mambo ya nje nchini Ujerumani na Nancy Faeser, anayesimamia masuala ya ndani nchini Ujerumani, walipozuru Uturuki jana Jumanne.

Kwenye kitita hicho, Uturuki itapokea euro milioni 33 na Syria itapokea euro milioni 17. Jeshi la Ujerumani imeshasafirisha zaidi ya tani 340 ya misaada kwa Ukraine. Mnamo Jumanne, jeshi la angani la Ujerumani lliratibiwa kusafirisha tani 13 zaidi ya misaada ikiwemo mahema, vitanda na zaidi ya mifuko 1,000 ya kulala.

NATO yapeleka makaazi ya muda Uturuki

Pamoja na misaada ya awali, kwa jumla Ujerumani imeshatoa kiasi cha euro milioni 108 kuwasaidia waathiriwa wa matetemeko ya Ardhi Uturuki na Syria. Baerbock amesema wanataka kuweka wazi kwamba kama jumuiya ya kimataifa, wanaliona janga hilo na wanawasaidia waathiriwa. Hata hivyo wakati mwingine wanakabiliwa na visiki hususan nchini Syria.

“Tunajaribu kukusanya misaada mingi kwa ajili ya Syria hususan kaskazini mwa nchi hiyo, kupitia njia ambazo zimefunguliwa, lakini utawala wa Syria unazidi kuzuia juhudi za Umoja wa Mataifa,” amesema Baerbock.

Idadi kubwa ya Waturuki walioko nje ya nchi yao wanaishi Ujerumani

Sehemu ya misaada ya Ujerumani kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi Uturuki na Syria
Sehemu ya misaada ya Ujerumani kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi Uturuki na SyriaPicha: Fabian Sommer/dpa/picture alliance

Ujerumani ina uhusiano maalum na Uturuki kwa kuwa ni nyumbani kwa idadi kubwa zaidi ya Waturuki wanaoishi nje ya nchi yao.

Waziri Faeser aliihakikishia kanda hiyo kwamba Ujerumani inashikana nao pamoja hasa wakati huu ambapo maelfu ya raia wao wameathiriwa.

UN: Dola bilioni 1 zahitajika kusaidia waathirika wa Uturuki

“Manusura ambao wamepoteza kila kitu wanahitaji kwa haraka nyumba za kuwakinga dhidi ya baridi kali,” alisema Faeser kabla ya kuanza ziara yao.

Ujerumani pia imeahidi kuwapa manusura makaazi katika taifa hilo la Umoja wa Ulaya.

Kulingana na mawaziri hao, jumla ya raia 96 wa Uturuki wameshakabidhiwa Visa kuwaruhusu kuingia Umoja wa Ulaya.

Visa hivyo vya miezi mitatu vinatolewa kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi, ili kuwawezesha kuishi na jamaa zao walioko Ujerumani kwa muda mfupi.

Idadi ya waliokufa yakaribia 50,000

Jimbo la Aleppo nchini Syria ni miongoni mwa maeneo yaliyotikiswa na tetemeko hilo la ardhi na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.
Jimbo la Aleppo nchini Syria ni miongoni mwa maeneo yaliyotikiswa na tetemeko hilo la ardhi na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.Picha: Muhammed Said/AA/picture alliance

Mnamo Februari 6, matetemeko mawili makubwa ya ardhi yalitikisha kusini mashariki mwa Uturuki na vilevile kaskazini mwa Syria. Zaidi ya watu 48,000 wameshafariki kutokana na janga hilo huku Uturuki pekee ikirekodi vifo vingi zaidi vya ya watu 42,000.

Siku moja kabla ya ziara ya Baerbock na Feaser, matetemeko mawili mapya yenye ukubwa wa 6.4 na 5.8 kwenye vipimo vya ritcha pia yalikumba Uturuki na Syria. Watu sita waliripotiwa kufariki na mamia walijeruhiwa.

Baerbock na Faeser walitembelea pia mji wa Gaziantep, ambapo wanatumai kukutana na wafanyakazi wanaotoa misaada, na mashirika yasiyo ya serikali yanayofanya kazi Uturuki na Syria.

Katika jimbo ambalo limeathiriwa vibaya la Kahramanmaras, mawiziri hao watazungumza na waathiriwa wa matetemeko hayo pamoja na wasamaria wema.

Kabla ya kurudi nchini mwao, Baerbock na Faeser pia wamepanga kutembelea kituo kipya cha maombi ya visa katika mji wa Gazientep.

(Vyanzo: AFPE, DPAE, RTRE)