1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa chama cha siasa BSW Ujerumani waipinga AFD

Iddi Ssessanga
4 Juni 2024

Kiongozi wa zamani wa wabunge wa chama cha kisoshalisti cha mrengo wa kushoto, Die Linke na mwanasiasa mkongwe Sahra Wagenknecht, hivi sasa anaendesha chama kipya kilichopewa jina lake.

https://p.dw.com/p/4gdc5
Ujerumani |Siasa | Sahra Wagenknecht | BSW
Mwanasiasa mkongwe nchini Ujerumani na Mkuu wa chama kipya cha siasa BSW Sahra Wagenknecht.Picha: Focke Strangmann/dpa/picture-alliance

Wachambuzi wanasema chama cha siasa za mrengo mkali wa kulia cha AfD ndicho kinapaswa kuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na chama hiki kipya kinachojulikana kwa kifupi kama BSW. 

Wakati mwanasiasa mashuhuri wa mrengo wa kushoto Sahra Wagenknecht alipotangaza kuwa anaanzisha chama chake mwaka jana, baadhi walikitaja chama hicho kuwa mbadala kwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD, na kwamba chama hicho kilikuwa na sababu kubwa ya kuwa na wasiwasi.

Wachambuzi wa siasa wamekuwa wakihoji kuwa msimamo wa kipekee wa Muungano wa Sahra Wagenknecht (BSW) - wa mrengo wa kushoto kwenye masuala ya kiuchumi, lakini unaokaribiana na chama cha AfD kwenye masuala kama vile uhamiaji na tofauti za kijinsia - unaweza kuleta tishio kwa AfD.

Soma pia:Utafiti: Wajerumani wachache kujitokeza uchaguzi wa Ulaya

Uchaguzi wa Ulaya wa Juni 9 utakuwa moja ya mitihani mikubwa ya kwanza ya nadharia hiyo.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin mwishoni mwa mwezi wa Aprili, Wagenknecht alielezea jambo lake mwenyewe kwa maneno yaliyopambwa vizuri, lakini rahisi. 

"Ni wazi kwamba tuna serikali ambayo haipendwi sana. Uchumi wa Ujerumani uko katika mgogoro, tumekuwa na mfumuko wa bei wa juu ya kiwango cha wastani,"

Alisema mwanasiasa huyo na kuvigeukia vyama vinavyounda serikali katika kufika suluhu ya changamoto hizo za kiuchumi na kijamii.

"Vyama vinavyounda serikali vimeshuka sana. Na bila shaka, hiyo imesababisha kuimarika kwa AfD na mrengo wa kulia."

Matokeo ya kujitenga na die Linke

Uamuzi wake wa kujitenga na Chama cha die Linke, ambacho kundi lake la wabunge aliwahi kuliongoza, ulipunguza uwakilishi wa chama hicho katika bunge la Ujerumani, Bundestag, baada ya kuhama na wabunge 10 kati ya 38 kilichokuwa nao, na huenda ukauwa kabisaa nguvu yake ya kisiasa katika siku zijazo.

Ujerumani | Siasa | Mwanasiasa Sahra Wagenknecht.
Mwanasiasa Sahra Wagenknecht akiwa katika kampeni za uchaguzi wa Bunge la Ulaya unaotarajiwa kufanyika Juni 9, 2024. Huu utakuwa ni uchaguzi wa kwanza kwa chama cha BSW.Picha: Focke Strangmann/dpa/picture-alliance

Wagenknecht alisema sababu iliyomfanya kukihama chama cha Die Linke ni kushindwa kwa chama hicho cha kisoshalisti kuwafikia watu wenye malalamiko, ambao wanataka mbadala wa kuaminika.

Kadhalika alikiri kwamba wanavua katika maji sawa na AfD, akinukuu tafiti kadhaa za maoni zinazoonyesha kuwa wapigakura wengi wa AfD ni wale wasioridhika na wanapiga kile kinachoitwa kura ya upinzani. 

Ingawa ameondoa uwezekano wa kuunda muungano na mrengo mkali wa kulia, baadhi ya sera zake zinafanana na za AfD.

Soma pia:Scholz: Hakuna hatari Ukraine kushambulia ndani ya Urusi kwa silaha za Ujerumani

BSW inapinga usafirishaji wa silaha Ukraine na vikwazo dhidi ya Urusi, na pia inataka kukataza mambo ya kijeshi ndani ya Umoja wa Ulaya na kuondoa silaha za nyuklia za Marekani.kutoka bara hilo.

Pia inataka suluhu la kidiplomasia katika vita vya Ukraine, ingawa Wagenknecht bado hajafafanua jinsi suluhu ya kidiplomasia inaweza kupatikana.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin mwezi Aprili, Wagenknecht alisema nchi za Magharibi zinaweza kujitolea kuacha kuipatia Ukraine silaha ikiwa Urusi itakubali kusitisha vita mara moja - jambo ambalo linaweza kuilazimisha Ukraine kuachia maeneo yanayokaliwa na Urusi.

Katika miaka ya hivi karibuni, yumkini hakuna mwanasiasa wa Ujerumani ambaye amekuwa mwiba mchungu kwa washirika na wapinzani kuliko Wagenknecht.

Kabla ya mgawanyiko wa mwaka jana, alisababisha hasira miongoni mwa wenzake wa Chama cha die Linke, ambao walikuwa wamechoshwa na nadhari ya vyombo vya habari aliopokea na ukaidi wake wa nidhamu ya chama.

Mtazamo wa wachambuzi kuhusu Wagenknecht

Baadhi ya wachambuzi wanasema Wagenknecht anatoa kitu ambacho hakijawahi kuonekana nchini Ujerumani: Maadili ya kihafidhina ya kijamii yanayofungamana na maadili ya kiuchumi ya ujamaa.

Utafiti: Kiwango cha Umasikini Ujerumani bado kipo juu

Mlinganisho wa karibu zaidi wa BSW kimataifa unaweza kuwa Chama cha Kisoshalisti (SP) nchini Uholanzi, ambacho pia kilichukua msimamo makali zaidi kuhusu uhamiaji, au Chama cha Kikomunisti cha Ugiriki (KKE), ambacho kilipiga kura kupinga mswada wa kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja.

Soma pia:Chama cha AfD kupata mafanikio katika uchaguzi wa Ulaya

Wagenknecht aliezaliwa  mwaka wa 1969 na mama wa Kijerumani na baba wa Kiirani mjini Jena, Thuringia, alitumia takriban maisha yake yote ya utu uzima katika chama ambacho sasa kinaitwa Chama cha Mrengo wa Kushoto - zamani kikijulikana kama Chama cha Umoja wa Kijamii (SED), chama cha kikomunisti kilichoitawala Ujerumani Mashariki.

Wachambuzi tayari wamekuwa wakichora ramani ya mapambano ya Wagenknecht: Ushiriki wa uchaguzi wa Ulaya wiki hii utafuatiwa na kampeni kamili katika majimbo matatu ya mashariki mwa Ujerumani baadae mwaka huu: Brandenburg, Saxony, na Thuringia.

Mustakabali wa kisiasa wa Ujerumani unaweza kwa kiasi kikubwa kutegemea mafanikio au kushindwa kwake.