Ujerumani na sera zake za siasa za kimataifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani na sera zake za siasa za kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amesema serikali mpya ya nchi hiyo inakusudia kujihusisha kwa kiasi kikubwa katika masuala makuu ya kimataifa ya sera zake za kigeni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier

Akilihutubia bunge mjini Berlin, jana Jumatano (29.01.2014) Steinmeier, amesema katika miaka ya hivi karibuni dunia imejionea mabadiliko makubwa na hivyo kutoa wito wa nchi hiyo kuongeza jitihada katika sera zake za kigeni.

Amesema mizozo mingi imekuwa karibu na Ujerumani na jinsi mizozo hiyo inavyoshughulikiwa au kutotiliwa maanani siku zote huleta madhara kwa Ujerumani, na bara la Ulaya limekuwa likijiangalia lenyewe tu, huku likipambana na mizozo na hivyo halipaswi kufumbia macho kile kinachotokea nje ya mipaka yake.

Steinmeier na Merkel wasisitiza kuhusu sera za kigeni

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel

Kwa pamoja Steinmeier na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel wamesisitiza kuhusu sera za nje na majukumu ya Ujerumani kwa Ulaya. Bibi Merkel alielezea jinsi nchi hiyo itakavyojihusisha katika kutatua mizozo miwili katika bara la Afrika.

Akizungumza na bunge katika hotuba yake kuhusu sera za nchi hiyo, Bibi Merkel alisisitiza yaliyoelezwa na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen, katika mahojiano yake na vyombo vya habari, kwamba Ujerumani inakusudia kupeleka wanajeshi wake katika nchi ya Mali na kuwaunga mkono wanajeshi wa Ufaransa walioko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Katika hotuba yake Merkel alisema moja ya nguzo nne za sera zake ni jinsi Ujerumani itakavyojihusisha na Ulaya pamoja na dunia nzima kwa ujumla na kuelezea umuhimu wa sera za kigeni na usalama, zitakazolileta pamoja jeshi na wataalamu wa kiraia. Merkel pia aligusia kuhusu suala la madai ya udukuzi uliofanywa na Marekani na kutoa onyo kali kwa nchi hiyo.

Aidha, Steinmeier amezungumzia mizozo inayoiandama dunia kwa sasa ikiwemo ile ya Mashariki ya Kati na ulimwengu wa Kiarabu, Ukraine na Afghanistan. Amesema pia eneo la Asia Mashariki linapaswa kuzingatiwa akigusia mzozo kati ya China na Japan.

Frithjof Schmidt, kutoka chama cha Kijani

Frithjof Schmidt, kutoka chama cha Kijani

Hata hivyo, chama cha upinzani cha Kijani cha watetezi wa mazingira nchini Ujerumani kimepinga kuhusu mpango wa sera hizo za kigeni za serikali. Frithjof Schmidt wa chama hicho amesema wanapinga kuhusu kulitumia jeshi kama chombo cha sera za kigeni na kwamba operesheni zote zinazoendelea lazima zisitishwe. Amesema suala la kuuza silaha nje ya nchi halikushughulikiwa ipaswavyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DW
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com