Ujerumani mguu mmoja katika kombe la dunia | Michezo | DW | 07.09.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani mguu mmoja katika kombe la dunia

Katika mechi zilizochezwa usiku wa kuamkia leo, mataifa vigogo wa soka barani Ulaya yamepiga hatua kusogelea kufuzu kushiriki katika michuano ya kombe la dunia itakayochezwa nchini Brazil mwaka 2014.

Miroslav Klose Philipp Lahm wakisherehekea goli

Miroslav Klose Philipp Lahm wakisherehekea goli

Timu ya taifa ya Ujerumani imewanyamazisha wapinzani wake wa jadi Austria kwa kuwazaba mabao 3-0 mbele ya mashabiki 68,000 katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich. Magoli hayo matatu kutoka kwa Miroslav Klose, Toni Kroos na Thomas Mueller yaliipeleka timu ya Ujerumani maarufu kama Mannschaft karibu na kufuzu kushiriki katika mechi za Kombe la dunia hapo mwakani.

Ushindi wa jana umeifanya Ujerumani ibakie kwenye kilele cha kundi C ikiongoza kwa pointi 5, huku zikibakia mechi tatu, ikiwemo ile itakayoikutanisha na vibonde wa kundi lao, yaani visiwa vya Faroe.

Klose aifikia rekodi ya Mueller

Goli alolifunga Miroslav Klose limemweka sabamba na Gerd Mueller kwa kuifungia Ujerumani mabao mengi

Goli alolifunga Miroslav Klose limemweka sabamba na Gerd Mueller kwa kuifungia Ujerumani mabao mengi

Goli alilolifunga Miroslav Klose mwenye umri wa miaka 35 lilikuwa lake la 68 kwa timu ya Ujerumani, idadi sawa na ile iliyofungwa na Gerd Mueller aliyekuwa akishikilia rekodi ya miaka 39 ya kuifungia mabao mengi timu ya taifa ya Ujerumani.

Tukio jingine la kihistoria katika mechi ya jana ni kuwa mechi hiyo ilikuwa ya 100 kwa nahodha wa timu ya Ujerumani Philipp Lahm, akiwa mchezaji wa nane nchini hapa kufikia hatua hiyo.

Sio Ujerumani peke yake iliyong'ara na kujiongezea matumaini ya kwenda Brazil mwaka kesho. Uingereza iliikandika Moldova magoli 4-0 na kusonga kileleni kwenye kundi H. Mawili kati ya magoli hayo yamefungwa na mshambuliaji wa Manchester United Dan Welbeck, ambaye hata hivyo mng'aro wake ulitiwa doa na kadi ambayo inamwondolea nafasi ya kucheza mechi inayofuata dhidi ya Ukraine, ambayo huenda ikatoa jibu kuhusu nchi gani kati ya hizo inakata tiketi ya moja kwa moja.

Uhispania waendelea kutesa

Nyota ya Jordi Alba inaendelea kung'ara

Nyota ya Jordi Alba inaendelea kung'ara

Mabingwa wa soka duniani na barani Ulaya, Uhispania, wameifunga bila taabu Finland kwenye uwanja wake kwa magoli yaliyowekwa wavuni na Jordi Alba na Alvaro Negredo, na kuipa kisogo Ufaransa ambayo wanagombania nafasi ya kwanza katika kundi I.

Ufaransa ambayo ililazimishwa sare tasa na Georgia inabakia katika nafasi ya pili kwenye kundi hilo. Na Italia inabebea kileleni kwenye kundi lake ikiacha kwa pointi saba Bulgaria inayoifuata, baada ya goli pekee lililoingizwa na Gilardino katika dakika ya 38, dhidi ya Jamhuri ya Czech mjini Turin.

Katika mechi nyingine zilizochezwa barani Ulaya, mkwaju wa penalti uliotingwa kimiani na Robin van Persie mnamo dakika za majeruhi umeisaidia Uholanzi kuambulia sare ya 2-2 na timu dhaifu ya Estonia.

Ronaldo aizamisha Ireland

Christiano Ronaldo, hat-trick yake imeizamisha Ireland ya Kaskazini

Christiano Ronaldo, hat-trick yake imeizamisha Ireland ya Kaskazini

Timu nyingine iliyojichimbia kileleni mwa kundi lake ni Ureno, ambayo nyota wake Christiano Ronaldo amefunga mabao matatu katika muda wa dakika 15, na kuigeuzia kibao Ireland ya Kaskazini ambayo ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1. Hadi kipenga cha mwisho ilikuwa Ureno 4, Ireland ya Kaskazini 2.

Ubelgiji na nahodha wake Vincent Kompany nao walijiweka katika nafasi nzuri kwa kuikandamiza Scotland mabao 2-0. Ushindi huo umeimarisha uongozi wa nchi hiyo katika kundi G, ambalo linazishirikisha pia Bosnia Herzegovina, Ugiriki, Slovakia na Liechtenstein.

Na huko nyumbani Afrika, Ghana imeichapa Zambia magoli 2-1 mjini Kumasi na kujihakikishia uongozi wa kundi D. Nchi hiyo ilihitaji pointi moja tu kujiunga na Algeria, Misri na Cote d'Ivoire katika kundi litakalocheza mechi za play-off, kuamua zile tano zitakazoliwakilisha bara la Afrika katika fainali za kombe la dunia. Timu nyingine tatu ambazo zitakamilisha safu ya play-off zitajufahamika baada ya mechi zitakazochezwa wikendi hii.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/AFPE

Mhariri:Caro Robi

DW inapendekeza