Ujerumani: Mawaziri wa nchi za nje wa G20 wakutana Bonn | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 16.02.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Ujerumani: Mawaziri wa nchi za nje wa G20 wakutana Bonn

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa mataifa makuu kiviwanda na yale yanayoendelea kiuchumi, yanayounda kundi la G20, wanakutana leo mjini Bonn-Ujerumani. Ni mkutano wa siku mbili utakaojadili maendeleo duniani.

Malengo ya maendeleo endelevu yaliyokubaliwa na jumuiya ya kimataifa yanatakiwa yawe yamefikiwa ifikapo 2030. Hali kadhalika kutambua na kuepuka mizozo katika siku zijazo pamoja na kulisaidia bara la Afrika, ni miongoni mwa masuala katika ajenda. Mawaziri hao wanakutana wakati pia ulimwengu ukikabiliwa na changamoto kuanzia  mabadiliko ya tabia nchi hadi vita nchini Syria, katika wakati wa misukosuko katika maeneo mbali mbali duniani.

Mbali ya nchi zilizoendelea kiviwanda, mataifa yanayoinukia na kupiga kasi ya haraka kiuchumi na ambayo ni wanachama wa kundi hilo ni China, India, Indonesia, Mexico, Afrika Kusini na Brazil.

Mkutano huo  utaanza  baadae mchana huu, lakini tayari mapema asubuhi kulifanyika majadiliano ya pamoja ya  maafisa wa kibalozi kutoka mataifa hayo 20, pamoja na wawakilishi wa mataifa kadhaa yalioalikwa. Hii itakuwa ni nafasi ya kwanza kabisa kwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Rex Tillerson, kukutana na wawakilishi wa mataifa muhimu katika ngazi ya kibalozi, wakiwemo mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi na na Uingereza, Sergei Lavrov na Boris Johnson na pia itakuwa ni nafasi ya kukutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Wang Yi, ambaye kuhudhuria kwake kulidhibitishwa siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano huo.

China Aussenminister Wang Yi (Reuters/G. Baker)

Waziri wa mambo ya nje wa China, Wang Yi

Kabla ya kuondoka Washington, msemaji wa  Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani, alisema mazungumzo  kati ya Tillerson na Lavrov kandoni mwa mkutano huo yatakuwa na umuhimu mkubwa, ambapon Tillerson atataka paweko na uhusiano utakaozingatia ukweli wa mambo ulivyo katika maeneo ambayo Marekani ina maslahi.

Mkutano huo wa G20 umeandaliwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel, mkosoaji mkubwa wa  misimamo wa  rais wa Marekani  Donald Trump kujilinda  kibiashara na ambaye ameonya kwamba  dunia iwe  tayari kukukabiliana na  hali ngumu chini ya utawala wake.

Waziri Gabriel amesema hakuna  nchi duniani itakayoweza kutatua matatizo makubwa ya kimataifa peke yake. Kundi hilo la G20 linahodhi karibu asilimia 85 ya uchumi wa dunia, kwa pamoja lina theluthi mbili ya wakaazi duniani.

Logo der deutschen G20 Präsidentschaft (Bundesregierung)

Nembo ya mkutano wa G20 wa Marais wa mjini Hamburg, Julai 2017

Pembezoni mwa mazungumzo hayo, Waziri Tillerson atakabiliwa na masuala kuhusu msimamo wa Trump kuelekea Umoja wa Ulaya ikiwa ni baada ya kuupongeza msimamo wa Uingereza wa kujitoa katika Umoja huo, huku akitabiri kwamba nchi nyengine zitafuata.

Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa G20, ni wa maandalizi ya mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa taifa na serikali utakaofanyika mjini Hamburg kaskazini mwa Ujerumani mwezi Julai. Huenda wakati huo, Rais wa Marekani, Donald Trump na Vladimir Putin wa Urusi, wakakutana kwa mara ya kwanza .

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp,ap,rtr

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com