Trump awasili mjini Brussels | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Trump awasili mjini Brussels

Rais Donald Trump amewasili Brussels, Ubelgiji akitokea nchini Italia ambako alikutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis. Trump anatarajiwa kukutana na rais wa Ubelgiji na viongozi wa Umoja wa Ulaya.

Belgien Trump in Brüssel (picture alliance/dpa/B. Doppagne)

Rais wa Marekani Donald Trump, Mfalme Philippe wa Ubelgiji na mke wa Trump Melania.

Kabla hajaondoka mjini Rome rais huyo wa Marekani Donald Trump, alisema mkutano wake na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ilikuwa ni heshima kubwa katika maisha yake na alieleza kupitia kwenye ujumbe wake wa Tweeter kuwa mkutano huo wa faragha uliofanyika katika maktaba binafsi ya Papa Francis, kiongozi huyo wa kanisa katoliki alimuhimiza Trump awe mtu wa kutafuta amani. Trump amesema ujumbe huo wa Papa Francis umemfanya awe na ari mpya ya kutaka kufuatilia zaidi amani ulimwenguni kuliko hapo awali. Trump alipokuwa akimuaga Papa Francis alimwambia kuwa hatasau maneno aliyomwambia.

Huku rais Trump na ujumbe wake wakiwa wamewasili mjini Brussels, Ubelgiji, Umoja wa Ulaya una matumaini kuwa mazungumzo ya Alhamisi baina ya viongozi wa Umoja huo na rais Donald Trump yatatuwama kwenye kuimarisha uhusiano baina ya Umoja huo na utawala wa rais Trump baada hofu kutanda juu hatma ya mkataba wa biashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya (TTIP) katika miezi ya mwanzo pale rais huyo wa Marekani alipoingia madarakani. Mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema hata kama sera za rais Trump zinatafautiana sana na za watangulizi wake, mawasiliano ya karibu na Umoja wa Ulaya lazima yaepuke kutoelewana kusiko na msingi juu ya mabadiliko ya masuala ya tabia nchi na masuala mengine ya kimataifa. Mogherini amesema anatarajia kusikia katika mkutano huo wa risala za kuendeleza juhudi zilizopo

Trump pia katika ziara yake ya nchini Italia alikutana na waziri mkuu wa nchi hiyo Paolo Gentiloni na baadae alikutana na rais wa Italia Sergio Mattarella. Katika ziara hiyo Trump aliandama na ujumbe wake akiwemo binti yake Ivanka ambaye pia ni mshauri wake.  Ivanka alikutana  na wanawake waliokombolewa kutoka kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kuwasafirisha watu kinyume cha sheria. Mkutano huo uliandaliwa na jamii ya Kanisa Katoliki la Sant'Egidio, mjini Rome.  Ivanka alisifu kazo inayoifanywa na jamii hiyo ya Kikatoliki aliwaambia nguvu ya kazi yao haionekani Rome tu bali inaonekana duniani kote. Aliisifu pia mipango mbalimbali iliyonzishwa na ambayo inaendelea kwa miaka mingi baadae. Ivanka alisema miradi hiyo imetoa misaada kwa wale waliokuwa wanahitaji zaidi, iwe ni wazee, masikini au wahanga waliosafirishwa kinyume cha sheria kutoka barani Afrika na kwengineko.

Mke wa rais wa Marekani, Mellani Trump alitembelea hospitali ya watoto ya Vatican ambapo alichora na kupiga picha pamoja na watoto wagonjwa wanaotoka kwenye nchi tisa tofauti ambao wamelazwa kwenye hospitali hiyo. Rais Trump atarejea nchini Italia hapo kesho jioni kwa ajili ya kuhudhuria mkutano mkuu wa nchi 7 zinazoongoza kiviwanda G7 utakaofanyika kwa siku mbili Ijumaa na Jumamosi mjini  Sicily.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/APE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com