Trump aitumia Israel kutia mafuta katika moto
16 Agosti 2019Hatua hiyo ya kuwazuwia wabunge Rashida Tlaib wa jimbo la Michigan na Ilhan Omar wa jimbo la Minnesota kuingia Israel imechochea moto wa mpambano na chama hicho kuelekea taifa hilo la Kiyahudi ambao umekuwa ukiendelea kuwaka nchini Marekani, huku Trump akiupulizia kwa nguvu moto huo.
Trump amesherehekea na uamuzi wa Israel katika ukurasa wa Twitter na ameliweka suala hilo mahususi katika muktadha wa kisiasa: "Wawakilishi Omar na Tlaib ni sura ya chama cha Democratic, na wanaichukia Israel! " ameandika Trump.
Muda mfupi kabla ya uamuzi huo kutangazwa, Trump alitoa ishara ya kumzindua waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, akiandika katika ukurasa wa Twitter kwamba " Itakuwa kuonesha udhaifu wa hali ya juu " iwapo Israel itawaruhusu wanawake hao kufanya ziara nchini humo.
"Nahusika tu na msimamo kwamba wanawapinga Wayahudi na wanaipinga Israel. Nafikiri mambo waliyosema ni ya kuchukiza. Mna orodha, hili sio kosa la kwanza. Kile walichosema kuhusu Israel na Wayahudi ni kitu kibaya sana na wamekuwa taswira ya chama cha Democratic."
Faida za kisiasa kuelekea uchaguzi
Uungaji mkono kutoka vyama vyote katika bunge la Marekani Congress umekuwa msingi wa uhusiano baina ya Israel na Marekani tangu kuundwa kwa taifa hilo la Kiyahudi, na wakosoaji wa uamuzi wa jana Alhamis wamesema wana hofu kwamba Trump na Netanyahu wanatumia hali hiyo kwa ajili na faida ya kisiasa ya muda mfupi.
Netanyahu anakabiliwa na uchaguzi mwezi ujao, na Trump anakabiliwa na uchaguzi mwakani.
Tlaib na Omar , wabunge wawili waliochaguliwa hivi karibuni ambao ni waislamu , ni wakosoaji wa jinsi Israel inavyowafanyia Wapalestina. Walipanga kufanya ziara mjini Jerusalem na Ukingo wa Magharibi katika ziara iliyotayarishwa na shirika la Kipalestina kwa lengo la kuonesha madhila yanayowapata Wapalestina.
Kampeni ya kuisusia Israel
Isreal imeelezea kwamba wabunge hao wanaunga mkono kile kinachoelezwa kuwa ni vuguvugu linalojulikana kama "ususiaji, kutowekeza, vikwazo'', ama BDS, linalounga mkono Wapalestina. Israel , na wanasiasa wengi wanaounga mkono Israel , wanaamini BDS ni chuki dhidi ya Wayahudi na lina nia ya kuliharibu taifa hilo, kitu ambacho wapinzani wanakana.
Seneta kiongozi wa kundi la wachache bungeni Chuck Schumer wa New York , ambaye ni Myahudi aliyechaguliwa katika ngazi hiyo ya juu nchini humo na mmoja kati ya watetezi wakubwa, amesema hatua hiyo ya Israel "italeta madhara tu katika uhusiano kati ya Israel na Marekani na uungaji mkono kwa Israel barani Amerika, na akaongeza, kuwanyima fursa wabunge wa Marekani ni ishara ya udhaifu, na sio nguvu.