1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Hatua ya kutolewa nje mbunge yakosolewa

Admin.WagnerD2 Juni 2021

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania yameonya vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake waliopata fursa ya kuingia katika vyombo vya maamuzi kuwa vinachochea mfumo dume.

https://p.dw.com/p/3uKok
Tansania Parlament in Dar es Salaam | Job Ndugai, Sprecher
Picha: DW/E. Boniphace

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania yameonya vitendo vya udhalilishaji wanawake waliopata fursa kuingia katika vyombo vya maamuzi vinachochea mfumo dume wenye lengo la kutaka kuwavunja moyo washindwe kujitokeza kwa wingi kwenye masuala ya uongozi na siasa. Hatua hiyo inakuja baada ya mbunge mmoja wa kike kutolewa nje na spika wa bunge Job Ndugai kwa madai mavazi yake yalikuwa hayana staha. 

Huku mbunge huyo anayetambulika kwa jina, Condester Sichalwe kutoka Jimbo la Mombo, akipata uungwaji mkono na wengi, masharika ya kutetea haki za binadamu yanaona kitendo alichofanyiwa ni kama kizingiti kinachotaka kuwarudisha nyuma wanawake katika harakati zao za kisiasa.

Kikionekana kukerwa na kitendo hicho, kituo cha sheria na haki za binadamu, LHRC kimetahadharisha kuhusu matumizi mabaya ya sheria na kanuni kwa ajili ya kuwakandamiza wanawake.

Tansania Nationalversammlung 2018
LHRC imekosoa tafsiri ya vifungu kuhusiana na mavazi ndani ya bunge na kuonya kwamba hatua kama hizo zinachochea kupunguza ari ya wabunge wanawake.Picha: DW/S. Khamis

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga anasema maamuzi ya kumwamuru mbunge huyo kuondoka ndani ya ukumbi wa bunge yanaonekana kuwa na walakini mkubwa maana mavazi yake hayakuwa na kasoro yoyote.

"Ile nguo aliyokuwa amevaa ni nguo ambayo inasitiri, ni nguo yenye heshima,. Na nguo kama hizo zimekwishawahi kuvaliwa na naibu spika, zimeshawahi kuvaliwa na wabunge wengine, na hata yeye amekwishawahi kuvaa nguo kama hiyo. kwa hiyo sisi tunaona kwamba kanuni hizi ama zina changamoto ya tafsiri au mtu yoyote anaweza kutafsiri vazi la heshima maana yake ni nini au pia wanawake wanaonekana kama ni kitu ambacho kinaweza kudhalilishwa kwa namna yoyote ile" alisema Henga.

LHRC yaonya hatua kama hiyo itawaondolea ujasiri wanawake bungeni.

Tangu kutokea kwa tukio hilo, idadi ya watu wanaochangia hoja hiyo na kukosoa uamuzi huo imekuwa ikiongezeka huku wengine wakija na tafsiri zao zinazojaribu kuelezea mlolongo mzima na mwenendo wa mavazi kwa wabunge wanawake ndani ya bunge.

Hata hivyo, mashirika ya haki za binadamu yanaona kwamba iwapo matukio kama hayo yataendelea kuwakumba wabunge wanawake, huenda katika siku za usoni kukashuhudiwa mijadala mingi ndani ya bunge ikitawaliwa na wabunge wa upande mmoja yaani wanaume pekee.

Wabunge wanawake ndani ya bunge walionekana kutofurahishwa na hoja iliyoibuliwa Mbunge wa Nyang'wale Hussein Amar ambayo ndiyo ilisababisha mbunge huyo kutolewa nje na Spika Job Ndugai.

Hata hivyo, mbunge huyo alirejea tena bungeni na kuendelea na shughuli za bunge kama kawaida huku akiwa amevalia mavazi mengine.

George Njogopa.