SPD yataja mawaziri wake serikali ya mseto | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

SPD SERIKALINI

SPD yataja mawaziri wake serikali ya mseto

Chama cha Social Democrat SPD) cha Ujerumani kimetoa orodha ya mawaziri watakaoingia kwenye serikali ya mseto na muungano wa vyama vya kihafidhina unaoongozwa na Kansela Angela Merkel wa CDU/CSU.

Viongozi wakuu wa chama cha SPD - Andrea Nahles anayeongoza chama hicho bungeni, na kaimu mwenyekiti, Olaf Scholz - waliwataja mawaziri wanaoingia kwenye serikali mpya siku ya Ijumaa (9 Februari), ambapo Scholz mwenyewe, aliye sasa meya wa mji wa Hamburg, anakuwa sio tu waziri wa fedha, bali pia naibu kansela.

Waziri mpya wa ajira kwenye serikali mpya ya mseto ni Hubertus Heil, ambaye kwa sasa ni mbunge kwenye bunge kuu la shirikisho, Bundestag, akiwakilisha jimbo la kaskazini mwa Ujerumani la Lower Saxony. 

Chama cha SPD kinachukuwa wizara sita muhimu kwenye serikali ya sasa - mambo ya nje, fedha, sheria, kazi, familia na mazingira. Kwa mujibu wa mgawanyo wa wizara uliotangazwa leo, angalau nafasi moja imekwenda upande wa mashariki mwa nchi, ambapo Franziska Giffey, mwanasiasa mwenye umri wa miaka 39 kutoka mji ulio mpakani na Poland, Frankfurt an der Oder, na ambaye ni meya wa sasa wa wilaya ya Neukoelln ya mjini Berlin, ametangazwa kuwa waziri wa familia.

Awali wizara ya familia ilikuwa chini ya Katarina Barley, ambaye sasa anahamia kwenye wizara ya sheria inayowachwa wazi na Haiko Maas, anayebeba jukumu la kusimamia wizara ya nje ya Ujerumani.

Uongozi wa chama hicho umezigawa nafasi za uwaziri nusu-bin-nusu baina ya wanaume na wanawake, huku wizara ya mazingira ikienda kwa katibu mkuu wa SPD, Svenja Schulze, anayetokea jimbo lenye watu wengi zaidi hapa Ujerumani, North Rhine Westphalia.

Gabriel 'atemwa'

Sigmar Gabriel (Getty Images/S. Gallup)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani anayemaliza muda wake, Sigmar Gabriel.

Jana, waziri wa mambo ya nje anayemaliza muda wake, Sigmar Gabriel, aliarifiwa na viongozi wa chama hicho - mkuu wa SPD bungeni, Andrea Nahles, na kaimu mwenyekiti, Olaf Scholz - kwamba asingelikuwamo kwenye  serikali mpya, kama ilivyo kwa waziri wa mazingira anayemaliza muda wake, Barbara Hendricks.

Akiwa kwenye maonesho ya utalii mjini Berlin, Gabriel alizungumza kwa mara ya mwisho kwenye jukwaa la kimataifa akiwakaribisha na papo hapo kuwaaga wageni wanaohudhuria maonesho hayo.

"Kwa kuwa huu ndio mkutano wangu wa mwisho kimataifa, na pia mkutano wa mwisho na waandishi wa habari kuhusu masuala ya kimataifa, nina furaha ya kushirikiana na marafiki wema wa Ujerumani kwenye hili. Karibuni Ujerumani na nawatakia mafanikio kwenye maonesho haya ya utalii ya Berlin," alisema Gabriel.

Kwa upande wake, chama cha Christian Democratic Union (CDU) cha Kansela Merkel, kinachukuwa wizara za ulinzi, uchumi, afya, elimu na kilimo.

Mshirika wake, chama cha Christian Social Union (CSU) kinachukuwa wizara ya mambo ya ndani, usafiri na masuala ya dijitali na pia wizara ya maendeleo. 

Serikali mpya inatazamiwa kuapishwa Jumatano ijayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com