1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yatangaza makubaliano ya usalama, uchumi na Uturuki

Mohammed Khelef
22 Februari 2024

Somalia imetangaza mkataba wa ulinzi na Uturuki ambao unajumuisha pia msaada kwa bandari za taifa hilo la Pembe ya Afrika, katika kile kinachoonekana kama ni kuyazuwia makubaliano ya Ethiopia na Somaliland.

https://p.dw.com/p/4clE0
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.Picha: REUTERS

Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre, aliyaelezea makubaliano hayo yaliyoidhinishwa na baraza lake la mawaziri siku ya Jumatano (Februari 21) kama "ya kihistoria".

"Somalia itakuwa na mshirika, rafiki na kaka wa kweli kwenye jukwaa la kimataifa," alisema.

Uturuki ni mshirika muhimu kwa Somalia na mojawapo ya mataifa yanayowania kuwa na ushawishi kwenye taifa hilo ambalo lipo kwenye eneo la kimkakati kutokana na kuwa kwake na ufukwe mrefu wa Bahari ya Hindi, kuwa karibu na Ghuba ya Aden na kuwa mlango wa Bahari ya Shamu.

Soma zaidi: Rais wa Somalia adai Ethiopia ilijaribu kumzuia kuhudhuria mkutano wa kilele wa AU

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Uturuki italipa jeshi la pwani la Somalia mafunzo na vifaa ili liweze kuwa na uwezo wa kuilinda nchi hiyo "dhidi ya vitisho na ugaidi, uharamia na uingiliaji wa kigeni."

Mkataba huo, ambao ulisainiwa kwa mara ya kwanza na mawaziri wa ulinzi wa mataifa hayo mnamo tarehe 8 Februari, utachukuwa miaka kumi ya utekelezaji. 

Somalia Proteste gegen Waandamanaji wakipinga mkataba wa Somaliland na Ethiopia mjini Mogadishu.
Waandamanaji wakipinga mkataba wa Somaliland na Ethiopia mjini Mogadishu.Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

"Kwa Somalia, makubaliano haya yanaleta msaada mkubwa wa ulinzi na miradi ya maendeleo, ambapo kwa Uturuki unaipatia fursa ya kutanuwa ushawishi wake na kuimarisha nafasi yake barani Afrika," alisema Mohamed H. Gaas, mchambuzi anayeongoza Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Amani ya Raad mjini Mogadishu.

Mkataba wa Somaliland na Ethiopia

Ethiopia ilisaini makubaliano ya awali na Somaliland mnamo Januari Mosi, ambayo yalizusha ghadhabu kali mjini Mogadishu iliyosema iko tayari kwenda vitani naEthiopia, kwani inaizingatia Somaliland kuwa mamlaka yake. 

Kwa upande wake, Somaliland inasema Addis Ababa ilikubali kuutambua uhuru wake ili nayo iipatie bandari ya kuweka kituo chake cha kijeshi.

Bandari ya Berbera ya Somaliland.
Bandari ya Berbera ya Somaliland.Picha: ED RAM/AFP

Soma zaidi: Sissi aioya Ethiopia juu ya mzozo wake na Somalia

Yaliyomo kwenye makubaliano hayo hayakuwekwa hadharani, lakini Somalia inauchukulia mkataba kama huo kama kitendo cha uchokozi, ingawa Somaliland imekuwa ikijiendesha yenyewe kwa takribani miongo mitatu sasa.

Rais Hassan Sheikh Mohamud aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumamosi kwamba maafisa wa ngazi za juu wa Ethiopia walikuwapo Somaliland "kuandaa mazingira" ya kuutwaa mkoa huo.

Ethiopia haijazungumza chochote dhidi ya tuhuma hizo, lakini Waziri Mkuu Abiy Ahmedamepuuzia wasiwasi wa kuzuka kwa mapigano kati ya nchi hizo mbili, akiwaambia wabunge mapema mwezi huu kwamba hakuwa "na dhamira yoyote ya kwenda vitani dhidi ya Somalia."

Ethiopia yenye watu zaidi ya 120, ndilo taifa lenye watu wengi zaidi lisilo na mpaka wa bahari duniani. 


Chanzo: AP