1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Somalia adai alizuiwa kuingia kwenye mkutano wa AU

Zainab Aziz
18 Februari 2024

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, amedai kwamba walinda usalama wa Ethiopia walijaribu kumzuia kuingia kwenye mkutano wa kilele Umoja wa Afrika.

https://p.dw.com/p/4cXtc
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud
Rais wa Somalia Hassan Sheikh MohamudPicha: REUTERS

Wizara ya mambo ya nje ya Somalia imesema katika taarifa yake kwamba serikali imelaani vikali hatua ya Ethiopia ya kuwazuia wajumbe wake.

Katikati mbele: Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud na ujumbe wake katika mkutano wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia
Katikati mbele: Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud na ujumbe wake katika mkutano wa AU mjini Addis Ababa, EthiopiaPicha: MICHELE SPATARI/AFP

Somalia imetoa mwito kwa makao makuu ya Jumuiya ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa ifanye uchuguzi huru kuhusiana na madai hayo ikisema kuwa Ethiopia ilikiuka itifaki zote za kidiplomasia na za kimataifa.

Soma Pia: Antonio Guterres azihimiza Somalia na Ethiopia kusuluhisha tofauti zao

Hata hivyo Ethiopia imepinga madai hayo hayo na imesisitiza kuwa Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alikaribishwa vyema kwenye mkutano huo wa 37 wa Umoja wa Afrika. 

Billene Seyoum msemaji wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Ethiopia imempa rais Mohamud, heshima kamili sawa na wakuu wengine wa nchi waliokuja kwenye mkutano huo.

Seyoum amesema rais wa Somalia aliingia kwenye ukumbi wa mkutano isipokuwa walinzi wake wa usalma wa rais ndio waliozuiliwa wakati walipokataa ulinzi uliotolewa na Ethiopia kwa rais wa Somalia na badala yake wakajaribu kuingia kwenye ukumbi wa mikutano na silaha zao.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed AliPicha: Massimo Percossi/Ansa/ZUMA Press/IMAGO

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, ameongeza kusema kwamba Ethiopia kama nchi mwenyeji, serikali yake inawajibika kwa usalama wa Wakuu wote wa Nchi na Serikali wakiwa nchini humo.

Somalia na Ethiopia, ni nchi ambazo tayari zimetofautiana kuhusu makubaliano ya matumizi ya bahari kati ya Ethiopia na jimbo linalojitawala la Somaliland.

Somalia inailaumu Ethiopia kwa kukiuka uhuru na mipaka yake kutokana na makubaliano ya Januari na mosi kati ya Ethiopia na Somaliland.

Somaliland ilijitangazia uhuru wake mnamo mwaka 1991 katika hatua ambayo haitambuliwi na jumuiya ya kimataifa.

Makubaliano hayo yanahusu Somaliland kukubali kukodisha kwaEthiopia eneo lenye ukubwa wa  kilomita 20 katika pwani yake kwa muda wa miaka 50.

Ethiopia inataka kuanzisha kituo cha majini na bandari ya kibiashara katika pwani hiyo.

Kwa upande wake, Somaliland inaitakaEthiopia iitambue rasmi kama nchi huru, madai ambayo hayajathibitishwa na Addis Ababa.

Ethiopia, nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika na mojawapo ya mataifa makubwa zaidi yasiyo na bahari duniani ilijikuta haina eneo la pwani baada ya Eritrea kujitenga na kujitangazia uhuru wake mnamo mwaka 1993 baada ya vita vya miongo mitatu.

Ethiopia iliitumia bandari ya Eritrea mpaka pale nchi hizo mbili zilipoingia vitani mwaka 1998 hadi 2000, na tangu wakati huo Ethiopia imekuwa ikiitumia bandari ya Djibouti kusafirisha sehemu kubwa ya biashara zake.

Soma Pia:Sissi aioya Ethiopia juu ya mzozo wake na Somalia

Wakati Somaliland kwa kiasi kikubwa imekuwa na utulivu, Somalia imeshuhudia miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na uasi wa kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Chanzo: AFP