1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Ukimwi yaadhimishwa ulimwenguni

Thelma Mwadzaya1 Desemba 2008

Ni miaka 20 tangu siku ya Ukimwi kuadhimishwa kote ulimwenguni.Siku hii huadhimishwa ili kutathmini hatua zilizopigwa mpaka sasa katika vita dhidi ya Ukimwi.

https://p.dw.com/p/G6be
Mkurugenzi mkuu wa shirika la UNAIDS Peter Piot akielezea ripoti ya takwimu za UkimwiPicha: AP


Kwa mujibu wa wataalam changamoto kubwa ni kuhakikisha kuwa mataifa masikini yanakuwa na uwezo wa kupata tiba mujarab.Mpaka sasa hakuna chanjo yoyote dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi iliyovumbuliwa.Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya watu milioni 33 wameambukizwa virusi vya HIV kote ulimwenguni.


Kauli mbiu ya siku ya Ukimwi ulimwenguni mwaka huu ni kuongoza,kuwezesha na kutimiza ahadi.Kauli hiyo inaangazia uongozi katika nyanja zote za jamii unaotilia maanani suala la Ukimwi na vita dhidi yake.Hatua zimepigwa kwani mpaka sasa idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi vya HIV wanaweza kuendelea kuwa na maisha marefu zaidi yaliyo na afya nzuri.Hii inatokana na matumizi ya dawa za kumaliza makali ya Ukimwi zinazopatikana katika mataifa mengi zaidi kwa sasa.


Hata hivyo bado kuna changamoto zinazokabili vita dhidi ya Ukimwi kama anavyosisitiza mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Ukimwi UNAIDS Bwana Peter Piot.


Marekani ilianzisha mpango wa kupambana na Ukimwi PEPFAR mwaka 2003 kwa lengo la kusambaza dawa za kupunguza makali ya Ukimwi ARV katika eneo lililo kusini mwa jangwa la Sahara. Mpango huo wa PEPFAR unafadhili miradi ya tiba ya magonjwa ya Malaria,Kifua Kikuu na Ukimwi katika mataifa 15 yaliyo masikini kabisa ulimwenguni.Mataifa hayo yako barani Afrika.


Mataifa ya Kenya,Tanzania na Rwanda ni baadhi ya mataifa yanayopata ufadhili.Baadhi ya shughuli zinazofadhiliwa na PEPFAR zinajumuisha huduma za upimaji wa damu wa hiari ili kuhakikisha kwamba hali ya mtu ya HIV inafahamika mapema.


Mwezi Julai mwaka huu Rais Bush wa Marekani aliidhinisha mswada ulioazimia kuongeza kiwango cha fedha zitakazotumika katika mpango wa PEPFAR kutoka bilioni 15 hadi dola bilioni 48.Nchi ya Kenya iliadhimisha wiki nzima ya kutoa huduma ya vipimo vya virusi vya HIV.


Kwengineko Mkewe rais wa Ufaransa Bi Carla Bruni Sarkozy ameteuliwa kuwa balozi wa mfuko wa kupambana na malaria,Kifua Kikuu na Ukimwi ulimwenguni,Global Fund.Bi Sarkozy anajiunga na vita hivi kufuatia kifo cha kakake mwaka 2006 baada ya kuugua Ukimwi.Kampeni zake zitajikita zaidi katika kuzuia maambukizi ya mama hadi mtoto wakati wa uja uzito.


Mwezi Oktoba utafiti wa Ukimwi ulipata msukumo mpya baada ya wanasayansi wawili waliogundua virusi vya HIV kutuzwa nishani ya Nobel ya dawa.Hata hivyo juhudi za kuvumbua chanjo dhidi ya Ukimwi bado zinaendelea.