Kupatikana kwa chanjo ya Virusi vya HIV/ Ukimwi, Duniani. bado kimebaki kitendawili. | Masuala ya Jamii | DW | 11.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Kupatikana kwa chanjo ya Virusi vya HIV/ Ukimwi, Duniani. bado kimebaki kitendawili.

Kikao cha Umoja wa mataifa kinachojadili kuhusu juhudi za kupambana na maradhi ya Ukimwi na Virusi vya HIV kinaendelea nchini Marekani.

Muunguzi akimtoa mtu damu ili kupimwa virusi vya HIV, katika kituo kimoja huko San Salvador nchini El Salvador.

Muunguzi akimtoa mtu damu ili kupimwa virusi vya HIV, katika kituo kimoja huko San Salvador nchini El Salvador.

Katika Kikao hicho Marekani imeufahamisha Umoja wa Mataifa kwamba chanjo dhidi ya Virusi vinavyosababisha maradhi ya Ukimwi bado imebakia kitendawili ikiwa ni miaka ishirini na saba tangu kuzuka kwa Virusi hivyo na huwenda ikachukua miongo kadhaa.

Duru ya pili ya majadiliano kuhusu juhudi hizo za kupambana na Virusi vya HIV na maradhi ya Ukimwi, jana ilihamia kwa viongozi wa ngazi za juu wa Serikali.

Anthony Fauci, ni Mkurugenzi wa taasisi inayohusika na maradhi ya kuambukiza na matatizo ya Mzio ya Marekani, amekiambia kikao hicho cha Umoja wa Mataifa kwamba, Uchunguzi wa chanjo ya HIV, ulishindikana pia mwaka jana.

Amesema upatikanaji wa chanjo hiyo utachukua miongo na miongo wakati ambapo Virusi vinavyosababisha maradhi ya Ukimwi vimeonyesha kuwa virusi hivyo vinatofauti kubwa sana na virusi vya maradhi mengine ambavyo chancho zake zimeweza kupatikana.

Aidha amebainisha kuwa Virusi hivi vya HIV, ni virusi ambavyo huwezi kutabiri kwamba chanjo yake itapatikana lini ili kuweza kukinga maradhi hayo.

Amesema, hata yeye hawezi kutabiri ni lini chanjo ya ugonjwa huo itapatikana, lakini anasema huwenda ikachukua miaka kumi au pengine zaidi.

Waathirika wa kwanza waliogundulika kuwa na maradhi ya Ugonjwa wa Ukimwi walikuwa ni wanaume watano wanaofanya mapenzi ya jinsia moja huko San Francisco, ambao waliripotiwa na kituo cha kuzuia na kukinga magonjwa cha Marekani mnamo mwaka 1983.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni ishirini na tano tayari wameshapoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa Ukimwi, tangu wakati huo na zaidi ya watu milioni arobaini na mbili wanaishi na Virusi vya Ukimwi ulimwenguni.

Bwana Fauci, amesema kwamba kila mwaka nchini Marekani kumekuwepo na taarifa za maambukizi mapya ya ugonjwa huo kwa watu elfu hamsini na idadi imekuwa ikiongezeka zaidi ya miaka iliyopita.

Lakini Bwana Fauci, ambaye ni mwanasayansi wa muda mrefu anayejihusisha katika mapambano dhidi ya Virusi vya HIV na UKIMWI kwa miaka mingi sasa, amesema maambukizi hayo yamefikia kiwango cha juu na kiasi cha asilimia kumi na mbili ya waathirika wapya ni Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Amelitaja tatizo kubwa lililopo nchini Marekani kuwa ni upatikanaji wa nyenzo za matibabu.

Mkurugenzi huyo wa taasisi inayohusika na maradhi ya kuambukiza na matatizo ya Mzio ya Marekani, amesema maambukizi kwa upande wa Ulaya Magharibi yanafikia asilimia moja ya idadi ya watu katika kila nchi, wwakati Ulaya Mashariki ni zaidi ya asilimia moja.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, kumekuwepo na harakati mbalimbali za kuweza kufikia moja ya malengo yake ya kumaliza na kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi ifikapo mwaka 2015.

Lakini umoja huo umesema pia kwamba maambukizi haya mapya ya watu milioni mbili nukta tano katika kipindi cha mwaka jana, yamepita malengo ya utengenezwaji wa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo kwa waathirika katika nchi masikini.

Mwaka jana idadi ya watu waliopata dawa hizo za kupunguza makali inafikia milioni moja na katika kipindi cha mwaja jana pekee, kiasi cha dola bilioni kumi kilitumika katika mapambano ya ugonjwa huo sugu.

Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa uliitishwa kwa lengo la kupitia mikakati na hatua ambazo zimefikia mpaka sasa na kuangalia mbinu mpya za kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi ili kufikia malengo yake ifikapo mwaka 2015.

 • Tarehe 11.06.2008
 • Mwandishi Scholastica Mazula
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EHtd
 • Tarehe 11.06.2008
 • Mwandishi Scholastica Mazula
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EHtd
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com