siku ya chakula duniani | Habari za Ulimwengu | DW | 15.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

siku ya chakula duniani

Ulimwengu watakiwa kuongeza kilimo kupambana na tatizo la njaa

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon Mkurugenzi mkuu wa shirika la (FAO) Jacques Diouf,

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon Mkurugenzi mkuu wa shirika la (FAO) Jacques Diouf,

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameutolea mwito ulimwengu kushikamana kupambana na njaa duniani.Akizungumza katika mkutano wa kimataifa kuhusu usalama wa chakula huko Roma italia rais huyo wa Rwanda ameitaka dunia kuelekeza juhudi katika mikakati ya kuleta usalama wa chakula wakati ambapo takriban watu billioni moja wanakabiliwa na janga la njaa duniani.

Wakati ulimwengu ukijiandaa hapo kesho kuadhimisha siku ya chakula duniani, rais huyo wa Rwanda Paul Kagame ametoa mwito wa kuwepo mshikamo zaidi katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa chakula na hasa katika ulimwengu wa nchi zinazoendelea barani Afrika.Aliuliza swali katika kikao hicho cha Roma akisema ikiwa kila mmoja anafahamu kwamba njaa inaua na kuwaondolea watu hadhi zao sasa kwanini hapachukuliwi hatua zaidi kukabiliana nayo?

Wito wake amezitaka nchi zote duniani kuelekeza nguvu zao katika kupanga hatua zaidi za kuleta usalama wa chakula lakini pia ameonya kwamba wakulima wadogo wasitengwe bali wahusishwe zaidi katika kutafuta suluhisho. Zaidi ya hayo amezitahadharisha nchi za kiafrika ambako ndiko kwenye idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na njaa kwamba wasipotoshwe na kasumba kuwa sekta za binafsi ndizo zinazoweza kuchukua jukumu la kutatua tatizo hilo la njaa duniani-

Wakulima wadogo pamoja na familia zao wanawakilisha takriban idadi ya watu billioni 2 na nusu hii ikiwa ni zaidi ya thuluthi tatu ya idadi jumla ya watu duniani.Mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya chakula na kilimo FAO Jacques Diof amesema janga la njaa duniani ni kitisho cha usalama kwa jumla na kuzitaka serikali kuungana na kushirikiana katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo.

Diof ameweka wazi katika kikao hicho kilichoandaliwa na shirika la FAO mjini Roma kwamba kwa kila hali pana haja ya kufikiwa malengo ya millenium ya kupunguza idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kutoka idadi ya asilimia 20 ya mwaka 1990 hadi asilimia 10 kufikia mwaka 2015.

Shirika la FAO linakadiria kwamba watu millioni 925 wanakumbwa na baa la njaa ikilinganishwa na watu billioni zaidi ya moja mwaka jana kutokana na athari zilizosababishwa na kuporomoka kwa uchumi pamoja na kupanda kwa bei ya vyakula katika mwaka wa 2007 hadi mwaka 2008.

Aidha serikali zimetakiwa kuwasaidia wanawake ambao zaidi ndio wanaolima vyakula kwa wingi katika nchi zinazoendelea lakini haviwafaidishi.Wanawake pia wametakiwa kuwa mfano katika mapambano dhidi ya njaa duniani.

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE

Mhariri AbdulRahaman

 • Tarehe 15.10.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PfHi
 • Tarehe 15.10.2010
 • Mwandishi Saumu Ramadhani Yusuf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PfHi
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com